Friday, June 10, 2016

KISUKARI CHA UKUBWANI KINAWEZA KUTIBIKA - HAKIKISHA MWILI WAKO HAUNA MLUNDIKANO WA TINDIKALI




Mwili wako umejaa tindikali?

Moja ya sababu kubwa za kisukari cha ukubwani ni mwili kujaa tindikali.

Tindikali ni nini?

Tindikali ni kitu chochote ambacho kinaongeza wingi wa atomu za hewa ya hydrogen zilizobeba umeme chanya [hydrogen ions (H+)] katika kimiminika chochote.  Atomu ni kipande kidogo kuliko vyote katika kiasili (chemical element) fulani cha kikemia ambacho hakijapoteza tabia za kikemikali za kiasili hicho.
Uzimuaji wa tindikali

Kitu chochote chenye uwezo wa kuzimua tindikali, kwa maana ya kupunguza idadi au kuondoa  kabisa kiasi cha wa atomu za hewa ya hydrogen zilizobeba umeme chanya, kinaitwa alkali. Kwa kawaida alkali mbalimbali huwa zinasababisha kupatikana kwa chembechembe za kikemia zilizobeba umeme hasi zinazoitwa [hydroxl ions (OH-)] pale alkali hiyo inapochanganywa na maji.  

Je, kitu hiki ni tindikali au ni alkali?

Kipimo cha kupima udhaifu au ukali wa kitu kwa munasibu wa utindikali au ualkali wake kwa kitaalamu kinaitwa pH. Herufi hizi ni kifupi cha ‘potential of Hydrogen’, ikiwa na maana ya ‘wingi wa hydrogen’. Mzani wa kupimia pH ya kitu chochote umegawanywa katika vipimo vidogo vyenye tarakimu kuanzia 0.00 hadi 14.00. Nambari 7.00 inawakilisha pH ya kitu chochote kilichozimuliwa (neutral). Tarakimu yoyote chini ya nambari 7.00 na kushuka hadi 0.00 inawakilisha utindikali wa kitu na tarakimu yoyote juu ya nambari 7.00 na kupanda hadi 14.00 inawakilisha ualkali wa kitu.

Kadri nambari inavyozidi kuwa ndogo kutoka 7.00 ndivyo ukali wa tindikali unavyozidi na kadri nambari inavyozidi kuwa kubwa kutoka katika 7.00 ndivyo ukali wa alkali unavyozidi.

Asili ya maumbile yetu

Katika maumbile ya asili ya mwanadamu, sehemu pekee yenye vimiminika vyenye tabia ya tindikali ni kwenye mfuko wa tumbo. pH ya kwenye mfuko wa tumbo ni kati ya 1 -3, lakini mara nyingi inakaribiana zaidi na 2.  Hii inaonyesha kuwa tindikali iliyoko tumboni ni kali sana!

Tunapozungumzia vimiminika mbalimbali yaliyoko mwilini, kuna haja ya kupima pH kwa ukamilifu zaidi na siyo kwa tarakimu nzima. Hii ni kutokana na ukweli kuwa katika ‘ulimwengu wa pH’ kuna tofauti kubwa sana kati ya tarakimu mbili nzima zinazofuatana. Kwa mfano pH ya 5.0 inaonyesha utindikali wenye ukali mara kumi zaidi kuliko pH ya 6.0, lakni pH ya 4.0 inaonyesha utindikali wenye ukali mara mia zaidi (10 x 10) kuliko pH ya 6.0! Hivyo basi mabadiliko kidogo sana katika pH mwilini yanawakilisha mabadiliko makubwa sana katika jinsi ambavyo mwli wako unafanya kazi.

Kwa kawaida pH  ya vimiminika mbalimbali mwilini mwako hubadilika badilika kulingana na kile kinachoendelea ndani ya mwili. Iwapo mabadilko katika pH yatakuwa makubwa sana au yatakuwa endelevu, basi mwili wako utakumbana na matatizo ya kiafya.

Vimiminika vilivyoko ndani ya mwili

Kuna vimiminika vya aina nyingi sana mwilini. Mwili wa mtu mzima mwenye umbo la wastani unabeba kiasi cha lita 40 za majimaji ya aina mbalimbali – damu, mate, nyongo, mkojo, ‘juisi’ za kongosho, nakadhalika. Kuna vimiminika ndani ya seli na nje ya seli, kama sehemu ya damu, kuzunguka viungio, ndani na kuuzunguka ubongo pamoja na uti wa mgongo, ndani ya viungo (organs) na kuvizunguka.

Kwa mujibu wa rejea mbalimbali za kitabibu, majimaji haya yote ukiondoa yale yaliyoko kwenye mfuko wa tumbo yana au yanaweza kuwa na ualkali, yaani kuwa na pH zaidi ya 7.0.   Vifuatavyo ni viwango vya pH vya vimiminika mbalimbali vinavyokubaliwa kitabibu kuwa ni vya kawaida.
•      Damu………………………………………………………………  7.35 -7.45
•      Vimiminika vya uti wa mgongo (spinal fluid)……………………    7.30 – 7.50
•      Mate (saliva)………………………………………………………   6.50 -  7.50
•      Vimiminika vya tumboni (gastric fluids)………………………        1.00 – 3.00
•      Vimiminika vya utumbo mwembamba (duodenum)…………….     4.20 – 8.20
•      Haja Kubwa (feses)…………………………………………………            4.60 – 8.40
•      Mkojo (urine)………………………………………………………  4.80 – 8.40
•      Kongosho (pancreas)………………………………………………  8.00 – 8.30
•      Nyongo iliyozalishwa na ini (Liver bile)……………………………7.10 – 8.50
•      Nyongo iliyohifadhiliwa kwenye kifuko cha nyongo (Gall Bladder Bile)………………………………………………………...........     5.50 – 7.70
           
Kwa kutazama jedwali hilo hapo juu utaona kuwa vimiminika vyote mwilini ukiondoa vile vya mfuko wa tumbo vinapaswa kuwa na ualkali, yaani vikipimwa, kipimo cha pH kitasoma juu ya 7.00. Kama hali ndiyo hii, ni kwa nini basi baadhi ya viungo nyeti sana, katika hali halisi, vinakuwa vimebeba au vinazalisha vitu vyenye utindikali wa hali ya juu?

Ni rahisi kuelewa ni kwa nini vimiminika vya mfuko wa tumbo vina utindikali mkali (pH ya kati ya 1.00 na 3.00). Vimiminika hivi vina kazi kubwa ya kulainisha ‘vitu vigumu’ (vyakula) kama moja ya hatua za awali  za kuchuja na kufyonza virutubisho kwa ajili ya matumizi ya mwili.   Lakini kwa nini kuwe na kutofautiana sana katika upeo wa pH kwa baadhi vimiminika ndani ya mwili, hususan vile ambavyo kimsingi vinapaswa kuondolewa mwilini mara kwa mara, mathalani mkojo na kinyesi? Ni kitu gani kinaweza kusababisha mkojo uwe na upeo wa pH ya 4.8 inayoashiria utindikali mkali na wakati mwingine pH ya 8.4 inayoashiria ualkali wa wastani? Lakini lililo muhimu zaidi ni kujiuliza: Ni kitu gani kinasababisha kupanda huku na kushuka kwa pH (fluctuation), kuwe ni kwa lazima? 

Mchango wa Lishe, Msongo na Mchakato wa Kawaida wa Kuishi

pH  haiwezi kubadilika bila kuwa na kichocheo (stimulus). Aghalabu kichochocheo huwa ni kitu tulichokula au msongo (stress), na kwa kiasi fulani mchakato wa kawaida wa kuishi. 

Lishe

Japokuwa vyakula vingi si tindikali pale vinapoingia kwenye vinywa vyetu, jivu la vyakula hivyo linalobaki baada ya mchakato wa kutoa nishati iliyomo kwenye vyakula hivyo kwa ajili ya matumizi ya mwili, ni lenye asili ya utindikali. Utindikali huu huathiri pH ya vimiminika vilivyoko mwilini ambayo huanza kushuka. Kama chakula unachokula kinaacha jivu la tindikali kali, ni suala la muda tu kabla ya vimiminika vya seli za mwili wa wako na vile vilivyomo kwenye mazingira ya nje ya seli kuelemewa na tindikali hiyo.

Msongo

Hali ni hiyo hiyo unapokabiliwa na msongo. Msongo ni kitu kinachounguza nishati nyingi sana ya mwili pamoja na kuchochea mabadiliko mengine mengi katika mchakato wa uvunjifu na ujenzi wa kemikali mwilini (metabolic processes). Vitendo hivi huzalisha tindikali nyingi ndani ya mwili ambayo pia huchangia pH ya vimiminika vilivyoko mwilini kushuka.

Mchakato wa Kawaida wa Kuishi

Shughuli mbalimbali za viungo vya mwili hutumia nishati. Matumizi haya ya nishati huzaa hewa ukaa (carbon dioxide). Hewa ukaa inapochanganyika na majimaji huzaa tindikali dhaifu ya carbon (carbonic acid). Pamoja na udhaifu wake tindikali ya carbon nayo pia inauwezo wa kuchangia pH ya vimiminika vilivyoko mwilini kushuka.

Mwili unajiteteaje?

Kama tulivyokwisha ona, asili ya vimiminika vingi ndani ya mwili ni kuwa katika hali ya ualkali.  Kwa sababu hii mwili una mifumo ya kujaribu kuondoa tindikali inayozalishwa mwilini ili isije ikabadili mazingira haya. Kuna mifumo mikuu miwili inayotumika kufanya kazi hii. Mfumo wa kwanza ni ule wa njia ya haja (hususan haja ndogo). Mara nyingi jivu la tindikali linalotokana na chakula, na tindikali inayozalishwa mwilini kutokana na msongo, huondolewa kwa njia hii. Kabla ya tindikali hii kutolewa mwilini huzimuliwa kwanza na madini ya alkali yaliyoko katika mfumo wa kiorganic (yalitokana na viumbe hai) ambayo yako mwilini kutokana na vyakula tunavyokula vyenye madini hayo, yaani matunda na mboga mboga za majani. 

Mfumo wa pili ni ule unaohusisha kupumua. Kupitia kupumua, tindikali dhaifu ya hewa ukaa inayotokana na utendaji wa kila siku wa viungo vya mwili  hutolewa nje.
Athari za upungufu wa madini ya alkali

Kutokana na watu kutozingatia kanuni za lishe sehemu kubwa ya lishe yao ni ile inayozalisha jivu jingi la tindikali ndani ya mwili. Hali hii hupelekea kupungua sana na hata kwisha kwa kiasi cha madini ya alkali yaliyoko mwilini. Hali hii ikitokea tindikali iliyoko mwilini inaweza ikaunguza vibaya sana njia ya mkojo wakati wa kuitoa. Ili hili lisitokee mwili ’huwasha’ mifumo ya dharura (backup systems) ya kuizimulia hiyo tindikali. 

Awali mwili kwa kutumia chembechembe za kiasili cha Nitrogen zilizoko mwilini (kutoka kwenye vyakula vya protini), utazalisha gesi ya Ammonia. Gesi hii ina ualkali wa hali ya juu na itatumika kuzimulia tindikali kabla ya kutolewa nje na mkojo. Hii ndiyo sababu kuna wakati mtu unakojoa mkojo wenye kutoa harufu kali ya kukereketa. Mkojo unakuwa umechanganyika na kiasi kikubwa cha ammonia na ammonia ni yenye harufu kali ya kukereketa.

Mfumo wa pili wa dharura ni ule unaotumia madini ya kalisi (calcium) kutoka katika mifupa. Iwapo pamoja na mwili kuzalisha ammonia ili kuzimua tindikali bado tindikali hiyo itaendelea kuwa nyingi ndani ya mwili, basi mwili huwasha mfumo wa pili wa dharura, ambao ni ule unaohusisha madini ya kalisi kuyeyuka kutoka katika mifupa na kuingia katika mzunguko wa damu ili yatumike kuzimulia hiyo tindikali.

Uwashaji wa mifumo hii ya dharura ni katika jitihada za mwili kuhakikisha kuwa upeo (range) wa pH ndani ya seli za mwili unabaki kuwa mdogo kadri inavyowezekana. Ili haya yawezekane baadhi ya viungo vya mwili hulazimika kufanya marekebisho ya jinsi vinavyofanya kazi. Kwa bahati mbaya marekebisho haya yanapokuwa ni ya kudumu hubadili utendaji wa mifumo ya mwili, na mabadiliko haya yanaweza yakazaa maradhi mbalimbali.
.  
Je, ni upi uhusiano kati ugonjwa wa kisukari na mlundikano wa tindikali mwilini?

Kama tulivyokwisha ona, mzigo wa tindikali unaotokana na vyakula (hususan vile vya jamii ya protini na wanga) ni lazima uzimuliwe kabla ya kutolewa nje ya mwili. Sehemu kubwa ya mfumo wa uzimuaji wa hii tindikali ni ule unaohusisha magadi (sodium bicarbonate) yanayozalishwa na kongosho. Kama mwili una madini ya sodium ya kiorganic ya kutosha kutokana na lishe, malighafi ya kuzalisha magadi mwilini ni ya kutosha na kongosho litafanya kazi yake kwa ufanisi.

Inapotokea kuwa malighafi ya kuzalishia magadi haitoshi, hali ya tindikali huanza kulemea viungo mbalimbali vya mwili, ikiwa ni pamoja na kongosho lenyewe. Kongosho ambalo kwa kawaida linatakiwa lifanye kazi katika mazingira yenye pH ya 8.0 – 8.30 hushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu pH ya mazingira yake imeshuka. Kinachofuatia ni kwamba majukumu muhimu ya kongosho yanaathirika, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa hormone ya Insulin ambayo ni muhimu katika uchakataji wa sukari ya kwenye damu.
Chukua hatua kukwepa janga la tindikali.

Moja ya hatua muhimu na isiyokwepeka unapotaka kuondokana na mzigo wa tindikali ndani ya mwili ni kurekebisha lishe yako. Ni muhimu kuzingatia kuwa katika makundi makuu ya vyakula, PROTINI NA WANGA huzalisha jivu la tindikali ndani ya mwili, na MBOGA ZA MAJANI NA MATUNDA (ukiondoa matunda aina ya creanberry) huzalisha jivu la alkali ndani ya mwili. Ni vizuri pia kuzingatia kuwa uwiano mzuri wa vyakula hivi kwenye mlo ni 80% MAJANI NA MATUNDA/20 PROTINI NA WANGA NA MAFUTA. KOZA.

Kurekebisha lishe yako na kuiweka katika uwiano huu ni hatua muhimu sana katika kutibu kongosho lako na hatimaye kuondokana na kisukari chako cha ukubwani.



KISUKARI CHA UKUBWANI KINAWEZA KUTIBIKA - KULA LISHE SAHIHI




Kisukari cha ukubwani ni nini?

Kisukari cha ukubwani ni hali inayojitokeza pale mwili wako unaposhindwa kuchakata sukari aina ya glucose na hivyo kuifanya ilundikane kwenye damu, badala ya kwenda katika seli za mwili ili itumike kuzalisha nishati ya kuendeshea shughuli za mwili. Mlundikano huu wa sukari kwenye damu una madhara mengi sana kiafya, kiasi kwamba hatua zisipochukuliwa kuondoa mlundikano huo kwenye damu, madhara hayo yanaweza kuishia kusababisha magonjwa hatari yanayoweza kupelekea kwenye ulemavu na kifo.

Magonjwa yenye uhusiano na mlundikano wa sukari kwenye damu ni yapi?

Baadhi ya magonjwa yenye uhusiano na mlundikano wa sukari kwenye damu ni shinikizo la juu la damu (hypertension), ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa figo, ugonjwa wa ini, uharibifu wa mishipa ya damu na ile ya fahamu, uharibifu wa macho, uharibifu wa ubongo, na maambukizi ya mara kwa mara ya vimelea vibaya vya maradhi hasa tumboni na kwenye njia ya haja ndogo. Aidha ni rahisi kwa mtu anayekabiliwa na mlundikano wa sukari kwenye damu kushindwa kupona majeraha na hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza viungo vya mwili, ikiwa ni pamoja na kupata upofu.

Sababu za kisukari cha ukubwani

Sababu za kisukari cha ukubwani ziko nyingi. Hapa tutazungumzia moja nayo ni kiungo kinachoitwa kongosho kushindwa kuzalisha homoni ya insulin ya kutosha. Insulin ndiyo homoni inayofanya kazi ya kubeba sukari na kuisafirisha kutoka kwenye damu na kuiingiza katika seli za mwili. Hii insulin inazalishwa na kundi la seli zinazopatikana kwenye kongosho zinazoitwa beta. Seli hizo zinaposhindwa kufanya kazi kwa sababu moja au nyingine kiasi cha isulin kinachozalishwa hupungua sana na hivyo kusababisha sukari ianze kulundikana kwenye damu.

Uharibifu wa kongosho.

Kumefanyika tafiti nyingi zilizolenga kubaini chanzo cha seli za beta kushindwa kazi. Baadhi ya hizi tafiti zimebaini kuwa maambukizi katika kongosho, hususan yanayotokana na virusi yanaweza yakaharibu seli hizi na hivyo zikaacha kufanya kazi. Hata hivyo tafiti nyingi zimebaini kuwa sababu kubwa ni uchovu. Tafiti hizi zimebaini kuwa kutokana na ulaji wa wanga uliopitiliza mipaka, hasa ule uliochakatwa (wali mweupe, sembe, chapati, mikate, chips, keki, sukari, soda, nakadhalika), seli hizi hupambana kuzalisha insulin ya kuondoa mzigo wa sukari unaoingia mwilini kila mara kupitia vyakula hivi, lakini hatimaye huzidiwa nguvu na kunyoosha mikono!

Kongosho linaweza kutibika!

Bahati nzuri tafiti zimebaini pia kuwa kisukari kinachokuja kutokana na mazingira haya kinaisha iwapo seli za beta zitapewa muda wa kutosha kupumzika. Imebainika kuwa seli hizi huanza tena kuzalisha insulin ya kutosha pale uchovu ziliokuwa nao unapomalizika. Ili kuzipumzisha seli zako za beta kuna haja ya kuondoa kabisa vyakula vinavyozalisha glucose kweye lishe yako. Miongoni mwa hivi ni hivyo tulivyotangulia kuvitaja katika paragraph iliyotangulia. Ili kupata nishati ya kutosha katika kipindi hiki utahitajika kuongeza kiasi cha mafuta bora ya kula kwenye kila mlo wako. Kumbuka mafuta bora zaidi ni yale ambayo ni koza (saturated fats) ikiwa ni pamoja na nazi, mafuta ya zaituni (olive oil), na siagi (butter). Mafuta ambayo siyo koza (polyunsaturated fats) kama yale ya alizeti yanaweza kufaa pia alimradi tu iwapo yataliwa katika hali ya ubichi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mafuta haya yanapopikia hubadilika na kutengeneza mafuta tenge (trans fats) ambayo tafiti zimebaini kuwa yanapoingia mwilini hulundikana kwenye mishipa ya damu na kuwa chanzo cha uharibifu mkubwa kwenye mfumo wa mzunguko wa damu. 

Muda wa kusubiri

Swali ni je, seli za beta hupumzika kwa muda gani kabla ya kuanza kufanya tena kazi? Muda wa haya mapumziko utatofautiana kati ya mtu na mtu kulingana na muda aliodumu na sukari yake kabla ya kuchukua hatua za kupumzisha hizo seli. Kwa bahati mbaya watu wengi huishi na mlundikano wa sukari kwenye damu kwa muda mrefu kabla ya kubainika kuwa ana tatizo hilo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa baadhi ya dalili za kuwepo kwa sukari nyingi kwenye damu zinaweza pia zikasababishwa na magonjwa mengine. Kwa bahati mbaya ni madaktari wachache wanaokumbuka kuwapima wagonjwa wao kisukari pale wanakutana nao. Hii inaweza ikapelekea mtu kuishi na kisukari muda mrefu sana kabla ya hatimaye kugunduliwa kuwa anacho.

Chukua hatua

Jambo la msingi ni kwamba kama unataka kuzuia usipate tatizo la kisukari au unataka tatizo hilo liondoke mapema kadri iwezekanvyo baada ya kubainika, basi unalazimika kuchukua hatua stahiki. Hatua hizi ni pamoja na:

1. Kupunguza sana ulaji wa vyakula tulivyotaja hapo juu. Hatua hii itakusaidia kujikinga na tatizo la kisukari katika maisha yako yote.

2. Kama huwezi kupunguza vyakula tulivyovitaja hapo juu, basi jitahidi kupima sukari walau mara moja kila baada ya majuma mawili. Hatua hii itakusaidia kugundua mapema kuwa tayari umeshapata tatizo na itakusaidia kuchukua hatua mapema za kuacha kula vyakula ambavyo vinalisumu kongosho lako. Kadri unavyochukua hatua mapema ndivyo itakavyokuwa rahisi kwa seli za beta katika kongosho lako kurejea katika hali yake ya kawaida.

3. Kama wewe tayari ni mgonjwa wa kisukari cha ukubwani na unataka upone na kuachana na matumizi ya kila siku ya dawa (ambazo aghalabu huwa na athari mbaya za pembeni), basi achana na ulaji wa vyakula tulivyotaja hapo juu. Hatua hii itaanzisha mchakato wa kupumzisha seli za beta za kongosho lako na kama zilikuwa hazijaharibika kabisa, baada ya muda zitarejea katika kufanya kazi kama kawaida.

Sasa tule nini?

Wagonjwa wengi wenye kisukari huishi maisha magumu sana, pale wanapotaka kuchukua hatua kuondokana na kisukari chao kwa njia ya kubadilisha lishe, hususan wanapokuwa mbali na makaazi yao. Tatizo ni kwamba jamii haijui kabisa kuwa ugonjwa wa sukari hivi sasa ni tatizo kubwa na kwa hivyo migahawa mingi haijaweka kabisa mazingira ya kuweza kuwahudumia watu wenye kisukari. Hata hivyo kama unajua aina ya chakula unachopaswa kula unaweza ukachukua hatua ya kuzungumza na hao wenye migahawa na walio wengi wako tayari kukusaidia.

Kwa ujumla mtu anayetaka kuachana na kisukari alichonacho anapaswa kula aina ya lishe inayoitwa ketogenic. Hii ni lishe ambayo hujumuisha protini kidogo, kiasi kikubwa cha mchanganyiko wa mboga za majani, na kiasi cha kutosha cha mafuta koza.

Protini kidogo tu yatosha!

Ni muhimu kuzingatia kuwa mwili hauhitaji protini nyingi. Kiasi kingi cha protini kina madhara kiafya kutokana na chakula hiki kuzalisha kiasi kikubwa sana cha tindikali ndani ya mwili. Baadhi ya taifiti zimeonyesha kuwa kiasi cha gramu 27 tu za protini kwa siku zinatosha. Hawa wanadai kuwa kuasi cha protini kinapozidi hapo mzigo wa tindikali mwilini unakuwa ni mkubwa mno kiasi kwamba mifupa ya mwili inaanza kuachia madini ya kalisi (calcium) kuingia katika mzunguko wa damu ili kusaidia kuzimua hiyo tindikali. Hata hivyo kundi kubwa la watafiti hupendekeza kati ya gramu 50 na 70 tu kwa siku. Vyakula vya protini ni pamoja na nyama (aina zote), maziwa, mayai, samaki, na wadudu kama senene, nakadhalika. Kuna baadhi ya vyakula ambavyo asili yake ni mimea ambavyo vimebea pia kiasi kikubwa sana cha protini. Hivi ni vile vya jamii ya kunde mathalani soya, maharage, kunde zenyewe, njegere, nakadhalika.

Sasa nitembee na mzani?

Ukweli wa mambo ni kwamba huhitaji kutembea na mzani. Hakikisha tu kwamba kiasi cha 80% ya nafasi katika sahani yako ya chakula kimechukuliwa na mchanganyiko wa mboga za majani, ikiwezekana 50% - 75% ya hizo mboga ziwe katika hali ya ubichi (vegetable salad). Katika ile 20% ya nafasi iliyobaki nusu inaweza kuchukuliwa na chakula cha protini chochote na nusu inaweza kuchukuliwa na mafuta koza yoyote uliyonayo.

KISUKARI CHA UKUBWANI KINAWEZA KUTIBIKA



KISUKARI CHA UKUBWANI – KANUNI YA MSINGI KATIKA KUJITIBU!

Kanuni ya msingi katika kujitibu kisukari cha ukubwani ni kufanya jitihada kudhibiti kiwango cha sukari kwenye mzunguko wa damu kibaki ndani ya wigo unaokubalika kwa kadri inavyowezekana. Sambamba na hilo jitihada zifanyike pia kuzuia uharibifu wa viungo muhimu vya mwili unaosababishwa na wingi wa sukari kwenye mzunguko.

Sukari ya ziada kwenye mzunguko wa damu husababisha madhara hata kwa wale ambao bado hawajapata ugonjwa wa kisukari. Sukari huongeza kasi ya kuzeeka kutokana na kuungana na protini za mwili kuzalisha kampaundi (compounds) zinazoitwa Advanced Glycation End Products, au kwa kifupi AGES. AGES husababisha protini husika kupoteza unyumbufu (supponess) na kukakamaa, pamoja na kukumbwa na mfuro (inflammation). Mchakato wa kuzalisha AGES huitwa glycosylation au glycation. Kadri kiwango cha sukari kwenye mzunguko wa damu kinavyokuwa kikubwa ndivyo mchakato huu unavyofanya kazi kwa haraka na kupelekea madhara yake kujidhihirisha.

Aghalabu AGES husababisha madhara makubwa ndani ya mwili. Mfuro uliosababishwa na Mchakato wa Glycosylation ni chanzo cha matatizo luluki ya kiafya ndani ya mwili.  Ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu, upofu, uharibifu wa figo na majeraha yasiyopona ni miongoni mwa madhara yanayoweza kusababishwa na huu Mchakato wa Glycosylation.

Moja ya protini zinazoathiriwa sana na sukari mwilini ni ile inayojulikana kama collagen. Collagen ni protini ambayo inatumika kama  malighafi kwa ajili ya kuundia tishu maalum zinazotimika kama kiungo au daraja baina ya tishu mbalimbali mwilini. Kitaalamu hizi tishu hujulikana kama connective tissues. Protini hii inapopata mfuro na kupoteza unyumbufu kutokana na sukari hupelekea tishu zinazoundwa nayo (connective tissues) kupungukiwa na uwezo wake wa kushikilia tishu nyingine. 

Hali hii huathiri uimara na utendaji wa viungo mbalimbali vya mwili kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano, mishipa ya damu ambayo kwa kiasi kikubwa imeundwa na collagen hupata mkakamo, na mkakamo huo huzaa ongezeko la shinikizo la damu na kusababisha msongo (stress) mkubwa kwa moyo. Msongo huu husababisha uharibifu wa misuli na mishipa ya moyo na hatimaye kuzalisha magonjwa mbalimbali ya moyo.   
Mchakato wa Glycosylation ni tatizo kubwa kwa wenye ugonjwa wa kisukari. Mchakato  huu ndiyo sababu kuu ya madhara yote ya muda mrefu yanayowakumba wagonjwa wa kisukari. Hii ni kwa sababu mchakato huu hutokea kwa kasi kubwa zaidi na kwa nguvu kubwa zaidi kwa wagonjwa wa kisukari kuliko wale ambao siyo wagonjwa.

Ukiondoa kusababisha Mchakato wa Glycosylation, sukari ya ziada kwenye damu pia huharibu mfumo wa mishipa ya fahamu, hususan ile iliyoko nje ya ubongo, uti wa mgongo na katika kivunge cha mishipa ya fahamu ijulikanayo kitaalamu kama ganglia. Sehemu ya mfumo wa mishipa ya fahamu inayoathiriwa na sukari kitaalamu huitwa peripheral nervous system. Uharibifu huu na ule wa mishipa ya damu kwa pamoja husababisha tatizo la gangrene, yaani kufa kwa kiasi kikubwa cha tishu, hususan katika baadhi maeneo ya miguuni. Macho na figo pia huathiriwa kwa kiasi kikubwa na huu uharibifu.

Tatizo lingine linalosababishwa na ulaji wa sukari na wanga ni ongezeko kubwa la ghafla la sukari kwenye mzunguko wa damu baada tu ya kumaliza kula. Kitaalamu ongezeko hili huitwa postprandial hyperglycemia. Tafiti zimethibitisha kuwa ongezeko hili la ghafla la sukari huharibu kuta za ndani za mishipa ya damu. Ili kuzuia hii hali baadhi ya madaktari hupendekeza matumizi ya dawa fulani fulani za kuzuia sukari kuingia kwenye damu kabla ya kula.

Utaratibu huu unashangaza sana. Haiingii akilini ni kwa nini mtu abugie sukari na wanga, kisha anywe dawa kuzuia asije akawa na ongezeko kubwa la sukari kwenye damu ambalo litamsababishia madhara. Ukweli wa mambo ni kwamba mgonjwa wa kisukari cha ukubwani akipunguza kula sukari na wanga baada ya muda fulani hahitaji kutumia tena dawa ya aina yoyote ile. Mgonjwa wa kisukari hatakiwi kupata hofu yoyote juu ya hili kwa sababu katika makundi yote makuu ya chakula, ni sukari na wanga pekee visivyo na ulazima kwa ajili ya kufanya maisha yadumu na kuendelea.

Wataalamu wa tiba za kisukari zisizokwenda sambamba na matumizi ya dawa za kifamasia wanasema hatua ya kwanza ni kupunguza kiasi cha wanga katika lishe. Kiasi cha gramu 60 za wanga au chini kidogo kwa siku kinapendekezwa.

Hatua ya pili ni kuzingatia ubora wa chakula. Chakula kinatakiwa kiwe kimejaza idadi kubwa ya viini-lishe kadri inavyowezekana. Hii ni kwa sababu baadhi ya hivi viini-lishe hutoa ulinzi dhidi ya uharibifu unaosababishwa na sukari. Nchi nyingi za bara la Asia zina historia ndefu ya kutibu kisukari kwa kutumia lishe. Kwa mfano, viungo vingi vinavyotiwa kwenye chakula nchini China huzuia ongezeko la sukari kwenye damu. Japokuwa huko nyuma watu walijifunza jinsi ya kutumia viungo hivi bila kujua jinsi vinavyofanya kazi ndani ya mwili, leo inafahamika kuwa viini-lishe vilivyoko katika hivi viungo hufanya kazi kwa kuzuia utendaji kazi wa kimeng’enya kinachoitwa alpha glucosidase. Moja ya majukumu ya kimeng’enya hiki ni kuchakata wanga na kuubadili kuwa sukari nyepesi ya glucose. Glucose ndiyo sukari inayolundikana kwenye damu baada ya kula sukari ya kawaida na wanga.  

Viini-lishe vinavyozuia utendaji kazi wa alpha glucosidase kwa kawaida huzuia ongezeko la ghafla la sukari kwenye damu, yaani postprandial plasma glucose. Kwa wagonjwa wa kisukari cha ukubwani viini-lishe hivi hupunguza ongezeko la sukari kwa kiasi cha 40 - 50 mg/dL (2.2 - 2.8 nmol). Miongoni mwa viini-lishe vinavyozuia utendaji kazi wa alpha glucosidase ni pamoja na vile vinavyojulikana kitaalamu kama anthocyanins, polyphenols, flavonoids, terpenoids na, curcuminoids. Hii ina maana kuwa viungo vingi, kwa mfano mdalasini, binzari nyembamba (jira), tangawizi, manjano, uwatu, na kalonji (black seed); mboga takriban zote za majani; mboga za jamii ya kunde; na  matunda kama maboga, parachichi, zambarau, karela (bitter gourd), papai, tikiti maji na nazi ni msaada mkubwa kwa wagonjwa wa kisukari, na wale wanaotaka kujikinga wasipate kisukari hicho.

UNAWEZA KABISA KUEPUKANA NA KISUKARI CHA UKUBWANI



CHIMBUKO LA KISUKARI NI CHAKULA KISICHOFAA!

Chakula ambacho ni bora kabisa kwa mtu mmoja, kinaweza kuwa sumu baridi kwa mtu mwingine, na kumletea madhara endelevu katika maisha yake. Kwa muktadha huu basi hakuna chakula bora kwa kila mtu! Chakula ni bora kwa mtu kama baada ya kukitumia mwili utakipokea vizuri, ukafyonza virutubisho, na kikasaidia kuimarisha afya ya huyo mlaji.

Ni vigumu kujua aina ya chakula inayokufaa, bila kujua jinsi mwili wako unavyochakata chakula. Kimsingi watafiti wamebaini makundi makuu matatu ya watu kuhusiana na jinsi miili inavyochakata chakula. Kundi la kwanza ni la wachakataji wa protini. Hawa miili yao inakubaliana zaidi na vyakula vya protini. Kwa watu wa kundi hili vyakula vya wanga, na hususan vile vilivyochakatwa na kuchujwa kwa kiwango kikubwa (highly processed and refined), ni sumu baridi ambayo itawapelekea kuugua maradhi mengi ya kimfumo.

Kundi la pili ni la wachakataji wa wanga. Hawa miili yao inakubaliana zaidi na vyakula vya wanga. Kwa watu wa kundi hili vyakula vya protini, na hususan vile vilivyochakatwa na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuwa na muda mrefu wa matumizi, ni sumu baridi ambayo itawapelekea kuugua maradhi mengi ya kimfumo. Kundi la tatu ni la wachakataji wa vyakula vya protini na wanga kwa viwango sawa. Kundi hili kidogo lina bahati kwa maana halidhuriwi kwa wepesi na vyakula vilivyoko katika yale makundi mawili ya mwanzo.

Moja ya magonjwa yanayosababishwa na mkanganyiko huu katika kula ni ugonjwa wa kisukari. Mchakataji wa protini anapokula chakula cha wanga, kasi ya kuchakata wanga huo ni kubwa mno ikilinganishwa na mlaji mwenzake ambaye ni mchakataji wa wanga. Kasi hiyo hupelekea kiwango cha sukari kinachoingia katika mzunguko wa damu ndani ya muda mfupi kuwa kikubwa sana. Kutokana na hali hii kongosho hulazimika kufanya kazi ya ziada kuzalisha kiwango kikubwa cha insulin (homoni ya kuondoa sukari kwenye damu na kuipeleka kwenye seli ili itumike kutengenezea nishati), ili kukabiliana na ongezeko hilo. 

Hali hii ikijirudia rudia mara kwa mara kongosho huchoka na kuanza kufanya kazi chini ya kiwango; au wakati mwingine vipokezi vya sukari katika seli (receptors) hushindwa kuendana na kasi ya kuletewa sukari kwa ajili ya matumizi ya seli, na huishia kuikataa sukari hiyo. Hali hii kitaalamu hujulikana kama insulin resistance, au pingamizi dhidi ya insulin kwa tafsri isiyo rasmi. Kuna baadhi ya nyakati yote mawili hutokea kwa wakati mmoja, yaani kongosho linafanya kazi chini ya kiwango, na pia mgonjwa anakabiliwa na pingamizi dhidi ya insulin.

Hivi karibuni imebainika kuwa moja ya sababu kubwa sana zinazopelekea vipokezi vya seli vikashindwa kupokea sukari inayoletwa ni kitu kinachoitwa mfuro (inflammation). Mfuro ni uvimbe kama lengelenge hivi. Mfano wa mfuro ni pale unapojikwaa au kujigonga usoni na mwili ukaumuka na kutengeneza nundu. Vichocheo vya kusababisha mfuro kwenye seli viko vingi lakini baadhi ya hivi ni vyakula tunavyokula kila siku. Vyakula hivi ni pamoja na sukari, wanga uiliochakatwa kwa kiwango kikubwa, na mafuta ya mbegu (alizeti, ufuta, karanga, pamba, mawese, nakadhalika) yanapotumiwa kwa ajili ya kupikia. Sababu nyingine ni maambukizi ya vimelea vya maradhi mbalimbali.

Wataalamu wameyagawanya magonjwa ya kisukari katika makundi makuu matatu. Makundi haya ni:
  1. Kisukari cha aina ya kwanza (type 1 diabetes). Hiki ni kisukari kinachojitokeza mapema (kwa kawaida kabla ya mtu kufika miaka 40), mara nyingi ikiwa ni katika kipindi cha utoto na ujana wa chini ya miaka 20. Katika aina hii ya kisukari mwili wa mhusika unaacha kuzalisha kabisa homoni ya insulin na hivyo kumlazimu mgonjwa kuishi kwa kudunga sindano za insulin kila siku.

  1. Kisukari cha aina ya pili (type 2 diabetes). Kiashiria kikubwa katika aina hii ya kisukari ni kwamba mwili hauzalishi insulin ya kutosheleza mahitaji, au vipokezi (receptors) vya sukari katika seli havifanyi kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wote wa kisukari duniani wanaugua aina hii ya kisukari.

  1. Kisukari cha ujauzito (gestational diabetes). Hiki ni kisukari kinachowakumba baadhi wanawake pale wanapokuwa wajawazito. Wakati  wa ujazito baadhi ya wanawake huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye mzunguko wa damu kuliko inavyotakiwa na wanaweza wakalazimika kutumia matibabu ili wasidhurike. Kutotambua kuweko kwa kisukari hiki na kukitibu kunaweza kusababisha matatizo wakati wa kujifungua. Moja ya madhara ya aina hii ya kisukari ni kuzaliwa watoto wenye miili mikubwa kuliko kawaida.

Kisukari ni ‘ugonjwa’ unaotisha. Ni ‘ugonjwa’ unaotisha kutokana na sifa zake. Sifa hizi ni pamoja na kutokuwa na dawa ya uhakika, kumlazimisha mgonjwa abadilishe mwenendo wake wa maisha kwa kiasi kikubwa, kusababisha mlolongo wa madhara mengine kibao ya kiafya ndani ya mwli, kuongeza gharama za maisha kwa mgonjwa, na ile hali ya kugeuka kuwa janga la kijamii.

Tunasema kisukari hakina dawa ya uhakika kwa kuwa ulimwengu wa tiba za kisasa umeshindwa kuja na dawa za aina hiyo hadi sasa. Dawa zilizoko ni zile za kumsaidia mgonjwa kushusha sukari iliyolundikana kwenye damu yake, ili iende katika viwango vinavyokubalika. Hata hivyo historia inaonyesha kuwa baadhi ya dawa hizi siyo salama, na hatima yake zinamsababishia mtumiaji madhara mengine ya kiafya ikiwa ni pamoja na kumwongezea uwezekano wa kupoteza maisha.

Avandia (rosiglitazone) ni moja ya dawa hizo. Mauzo ya dawa hii ambayo enzi zake ilikuwa ni moja ya dawa maarufu sana za kifamasia kwa ajili ua ugonjwa wa kisukari, yalifikia kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 3.2 mnamo mwaka 2006. Baada ya hapo ziliibuka taarifa za kitafiti kwamba dawa hii ilikuwa inasababisha madhara makubwa ya kiafya kwa mtumiaji kama vile ongezeko la hatari ya shambulizi la moyo (heart attack), wepesi wa kuvunjika mifupa na hususan ile ya mikononi juu ya kiwiko, uharibifu wa macho, kiharusi na uharibifu wa ini kutokana na ongezeko la sumu. Inakadiriwa kuwa ndani ya Marekani peke yake kati ya mwaka 1999 na mwaka 2006 dawa hii ilisababisha mashambulizi ya moyo (heart attacks) na vifo kati ya 60,000 na 200,000.

Japokuwa baadhi ya matatibu wa dawa za asili na zile za tiba mbadala wanadai kuwa wanatibu ugonjwa huu, madai haya yanapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari. Ni kweli kuwa mtu anaweza kuwa na dawa ya kuondoa sababu moja au zaidi ya kisukari na hivyo kumsaidia mtumiaji kuondokana na dalili zote za ugonjwa huo. Hata hivyo hii haina maana kwamba dawa hiyo itamtibu kila mgonjwa wa kisukari. Kwa kifupi ni kwamba kundi la wenye kisukari kilichosababishwa na sababu zinazoguswa na dawa husika watapona, na wengine wenye kisukari kilichosababishwa na sababu zisozoguswa na dawa hiyo hawatapona.

Mazoea yana tabu sana. Tulio wengi hatuli chakula kwa kuzingatia kanuni za afya bali tunakula kwa ajili ya mazoea na kulenga ladha. Mgonjwa wa kisukari mwenye nia ya kuidhibiti hali hiyo analazimika kuachana kabisa na kula kwa mazoea na kulenga ladha. Anatakiwa ajue kuwa vyakula vyote vya wanga, na hususan vile vilivyochakatwa kwa kiwango kikubwa, vina madhara makubwa kwake na anatakiwa kuviendea kwa tahadhari kubwa. Hali hii huwa ni chanzo kikubwa cha kufadhaika kwa baadhi ya watu ambao wamepata ugonjwa wa kisukari. Baadhi yao huuliza kwa ghadhabu : ‘sasa utakula nini???!’ na kuendelea kula vyakula vyao walivyozoea huku wakisaidiwa kisaikolojia na kimwili na vidonge wanavyopewa hospitalini na madaktari wao. Waathirika wengi wa madawa kama avandia ni wale wanaoangukia katika kundi hili.

Kisukari pia kinatisha kwa kuwa kinasababisha mololongo wa matatizo mengine kibao ya kiafya. Matatizo haya ni pamoja na uharibifu wa macho unaotambulishwa na magonjwa kama glaucoma (uharibifu wa neva za jicho), cataracts (ukungu kwenye lenzi ya jicho),  retinopathy (uharibifu mkubwa katika retina ya jicho), nakadhalika.  Matatizo ya miguu yanayotambulishwa na magonjwa kama neurapathy(maumivu yatokanayo na uharibifu wa mishipa ya fahamu), ulcers (vidonda sugu), gangrene (mkusanyiko wa tishu zilizokufa kutokana na kutofikiwa na mzunguko wa damu), nakadhalika. Matatizo mengine ni yale ya magonjwa ya ngozi na magonjwa ya moyo.

Faraja ya ugonjwa wa sukari ni kuufatilia kwa makini. Hii ina maana kuwa ni muhimu kufanya kipimo kila siku, ikiwezekana hata mara mbili au tatu kwa siku. Kutokana na hali hii gharama za kuufuatilia ugonjwa huu ni kubwa na huathiri kwa kiasi kikubwa hali ya kiuchumi ya mgonjwa. Kwa mfano tu, hivi sasa katika zahanati na vituo vingi vya afya, gharama za kupima kisukari kwa mara moja ni kati ya shilingi 2,000.00 na shilingi 2,500.00. Unapomwambia mtu apime mara tatu kwa siku maana yake atumie kati ya shilingi 6,000 na shilingi 7,500.00 kila siku!

Mwisho kisukari kinatisha kwa sababu taratibu kinaonekana kunyemelea hadhi ya kuwa ni janga kubwa sana la kijamii. Katika pande zote za dunia kisukari kinaongezeka badala ya kupungua. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, dunia inatarajiwa kuwa na wagonjwa wa kisukari 366,000,000 mwaka 2030 kutoka wagonjwa 171,000,000 waliokuwepo mwaka 2,000. Hili ni  ongezeko la aslimia 53! Tanzania, ambayo mwaka 2,000 ilikuwa na wagonjwa 201,600 inatarajiwa kuwa na wagonjwa 605,000 mwaka 2030, ikiwa ni ongezeko la 66.7%

Hata hivyo janga la kisukari linaoonekana kuzikumba zaidi zile nchi ambazo raia wao wanapendelea mno vyakula vya wanga katika mitindo tofauti- soda, pasta, doughnut, keki, mikate, lambalamba, nakadhalika. Nchi kama Italy uwiano kati ya Wataliano wanaoumwa kisukari na wale ambao hawaumwi ni 1:14!. Inawezekana sababu kubwa ikawa ni piza, pasta na spaghetti. Hivi ni vyakula vinavyotengenezwa kwa ngano na Wataliano wanavifakamia kwa wingi.

Marekani uwiano wao ni 1:17. Hii nayo ni jamii ambayo imelogewa soda, doughnut, chips, pizza, na vyakula vingine vya wanga vilivyochakatwa kwa kiwango cha juu. India uwiano wao ni 1:39. Hawa nao ni mabingwa wa vitu vitamu. Wahindi ni wafakamiaji wa tamutamu za kila aina na sifa kuu ya tamutamu hizi ni wingi wa sukari, ngano, mafuta na rangi.

Tanzania ina uwiano wa 1:238. Huu ni uwiano mzuri sana ukilinganisha na nchi tulizotangulia kuzitaja. Sababu ya uwiano huu mzuri ni nini wakati kimsingi sehemu kubwa ya Watanzania ni wala wanga zaidi kutokana na hali zao za kiuchumi? Nadhani sababu kubwa ni ukweli kwamba Watanzania wengi ni wakaazi wa vijijini na kimsingi pamoja na kwamba sehemu kuwa ya chakula chao ni wanga, lakini kutokana na sababu za kiuchumi, wanalazimika kuula wanga huo katika mfumo ambao haujachakatwa.

Kuepukana na ugonjwa wa kisukari ni muhimu kufanya kipimo cha kutambua aina ya mwili wako katika kuchakata vyakula (metabolic typing test) na iwapo utagundulika kuwa wewe ni mchakataji wa protini haraka uchukue hatua za kupunguza kwa kiwango kikubwa ulaji wa wanga, na hasa ule ambao umechakatwa kwa kiwango kikubwa. Nafasi ya wanga (kwa ajili ya kuzalisha nishati ya matumizi ya mwili) ichukuliwe na mafuta bora ya kula – nazi, siagi, samli, zaituni. Nafasi ya wanga kwa ajili ya kujaza tumbo ichukuliwe na mboga mchanganyiko za majani, na pale ambapo uwezekano upo, sehemu kubwa ya mboga hizo iwe mbichi (salad). Mafuta ya kawaida (yale tuliyoyazoea) tunaweza kuendelea kuyatumia (siyo kwa kupikia) bali kwa kupambia saladi (salad dressing). 

Aidha kama wewe tayari ni mgonjwa wa kisukari, utanufaika sana kwa kuondoa wanga uliochakatwa katika orodha ya vyakula vyako na ukaingiza wanga ambao haujachakatwa, tena kwa kiwango kidogo sana kma mbadala wake. Kwa ajili ya kuupatia mwili nishati punguzo hilo la wanga lichukuliwe na ongezeko la mafuta bora ya kula – nazi, siagi, samli, na zaituni. Aidha nafasi ya kushiba ichukuliwe na wingi wa mchanganyiko wa mboga za majani, ikiwezekana sehemu kubwa ya mboga hizi iwe mbichi (salad).

Kama ilivyo kwa yule anayelenga kukwepa kuugua kisukari, mafuta ya kawaida (yale tuliyoyazoea) tunaweza kuendelea kuyatumia (siyo kwa kupikia) bali kwa kupambia saladi. Ushauri huu kuhusu mafuta ni kinyume kabisa na ushauri mnaopatiwa na madaktari wenu kuhusu mafuta ya kula. Hata hivyo kisayansi ndio ushauri sahihi. Mungu akipenda post yetu ijayo itazungumzia jambo hili kwa kina ili kuliweka katika mazingira ya kueleweka zaidi..