CHIMBUKO
LA KISUKARI NI CHAKULA KISICHOFAA!
Chakula
ambacho ni bora kabisa kwa mtu mmoja, kinaweza kuwa sumu baridi kwa mtu
mwingine, na kumletea madhara endelevu katika maisha yake. Kwa muktadha huu
basi hakuna chakula bora kwa kila mtu! Chakula ni bora kwa mtu kama baada ya
kukitumia mwili utakipokea vizuri, ukafyonza virutubisho, na kikasaidia
kuimarisha afya ya huyo mlaji.
Ni vigumu kujua aina ya chakula inayokufaa, bila kujua jinsi
mwili wako unavyochakata chakula. Kimsingi watafiti wamebaini makundi makuu
matatu ya watu kuhusiana na jinsi miili inavyochakata chakula. Kundi la kwanza
ni la wachakataji wa protini. Hawa miili yao
inakubaliana zaidi na vyakula vya protini. Kwa watu wa kundi hili vyakula vya
wanga, na hususan vile vilivyochakatwa na kuchujwa kwa kiwango kikubwa (highly
processed and refined), ni sumu baridi ambayo itawapelekea kuugua maradhi mengi
ya kimfumo.
Kundi la
pili ni la wachakataji wa wanga. Hawa miili yao inakubaliana zaidi na vyakula
vya wanga. Kwa watu wa kundi hili vyakula vya protini, na hususan vile vilivyochakatwa
na kuhifadhiwa kwa ajili ya kuwa na muda mrefu wa matumizi, ni sumu baridi
ambayo itawapelekea kuugua maradhi mengi ya kimfumo. Kundi la tatu ni la wachakataji
wa vyakula vya protini na wanga kwa viwango sawa. Kundi hili kidogo lina bahati
kwa maana halidhuriwi kwa wepesi na vyakula vilivyoko katika yale makundi
mawili ya mwanzo.
Moja ya
magonjwa yanayosababishwa na mkanganyiko huu katika kula ni ugonjwa wa
kisukari. Mchakataji wa protini anapokula chakula cha wanga, kasi ya kuchakata
wanga huo ni kubwa mno ikilinganishwa na mlaji mwenzake ambaye ni mchakataji wa
wanga. Kasi hiyo hupelekea kiwango cha sukari kinachoingia katika mzunguko wa
damu ndani ya muda mfupi kuwa kikubwa sana. Kutokana na hali hii kongosho
hulazimika kufanya kazi ya ziada kuzalisha kiwango kikubwa cha insulin (homoni
ya kuondoa sukari kwenye damu na kuipeleka kwenye seli ili itumike kutengenezea
nishati), ili kukabiliana na ongezeko hilo.
Hali hii
ikijirudia rudia mara kwa mara kongosho huchoka na kuanza kufanya kazi chini ya
kiwango; au wakati mwingine vipokezi vya sukari katika seli (receptors)
hushindwa kuendana na kasi ya kuletewa sukari kwa ajili ya matumizi ya seli, na
huishia kuikataa sukari hiyo. Hali hii kitaalamu hujulikana kama insulin
resistance, au pingamizi dhidi ya insulin kwa tafsri isiyo rasmi. Kuna
baadhi ya nyakati yote mawili hutokea kwa wakati mmoja, yaani kongosho
linafanya kazi chini ya kiwango, na pia mgonjwa anakabiliwa na pingamizi dhidi
ya insulin.
Hivi karibuni
imebainika kuwa moja ya sababu kubwa sana zinazopelekea vipokezi vya seli
vikashindwa kupokea sukari inayoletwa ni kitu kinachoitwa mfuro (inflammation).
Mfuro ni uvimbe kama lengelenge hivi. Mfano wa mfuro ni pale unapojikwaa au
kujigonga usoni na mwili ukaumuka na kutengeneza nundu. Vichocheo vya
kusababisha mfuro kwenye seli viko vingi lakini baadhi ya hivi ni vyakula
tunavyokula kila siku. Vyakula hivi ni pamoja na sukari, wanga uiliochakatwa
kwa kiwango kikubwa, na mafuta ya mbegu (alizeti, ufuta, karanga, pamba,
mawese, nakadhalika) yanapotumiwa kwa ajili ya kupikia. Sababu nyingine ni
maambukizi ya vimelea vya maradhi mbalimbali.
Wataalamu
wameyagawanya magonjwa ya kisukari katika makundi makuu matatu. Makundi
haya ni:
- Kisukari cha aina ya kwanza (type 1 diabetes). Hiki ni kisukari kinachojitokeza mapema (kwa kawaida kabla ya mtu kufika miaka 40), mara nyingi ikiwa ni katika kipindi cha utoto na ujana wa chini ya miaka 20. Katika aina hii ya kisukari mwili wa mhusika unaacha kuzalisha kabisa homoni ya insulin na hivyo kumlazimu mgonjwa kuishi kwa kudunga sindano za insulin kila siku.
- Kisukari cha aina ya pili (type 2 diabetes). Kiashiria kikubwa katika aina hii ya kisukari ni kwamba mwili hauzalishi insulin ya kutosheleza mahitaji, au vipokezi (receptors) vya sukari katika seli havifanyi kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wote wa kisukari duniani wanaugua aina hii ya kisukari.
- Kisukari cha ujauzito (gestational diabetes). Hiki ni kisukari kinachowakumba baadhi wanawake pale wanapokuwa wajawazito. Wakati wa ujazito baadhi ya wanawake huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye mzunguko wa damu kuliko inavyotakiwa na wanaweza wakalazimika kutumia matibabu ili wasidhurike. Kutotambua kuweko kwa kisukari hiki na kukitibu kunaweza kusababisha matatizo wakati wa kujifungua. Moja ya madhara ya aina hii ya kisukari ni kuzaliwa watoto wenye miili mikubwa kuliko kawaida.
Kisukari ni ‘ugonjwa’ unaotisha. Ni ‘ugonjwa’ unaotisha
kutokana na sifa zake. Sifa hizi ni pamoja na kutokuwa na dawa ya uhakika,
kumlazimisha mgonjwa abadilishe mwenendo wake wa maisha kwa kiasi kikubwa,
kusababisha mlolongo wa madhara mengine kibao ya kiafya ndani ya mwli, kuongeza
gharama za maisha kwa mgonjwa, na ile hali ya kugeuka kuwa janga la kijamii.
Tunasema kisukari hakina dawa ya uhakika kwa kuwa ulimwengu
wa tiba za kisasa umeshindwa kuja na dawa za aina hiyo hadi sasa. Dawa zilizoko
ni zile za kumsaidia mgonjwa kushusha sukari iliyolundikana kwenye damu yake,
ili iende katika viwango vinavyokubalika. Hata hivyo historia inaonyesha kuwa
baadhi ya dawa hizi siyo salama, na hatima yake zinamsababishia mtumiaji
madhara mengine ya kiafya ikiwa ni pamoja na kumwongezea uwezekano wa kupoteza
maisha.
Avandia (rosiglitazone) ni moja ya dawa hizo. Mauzo ya dawa
hii ambayo enzi zake ilikuwa ni moja ya dawa maarufu sana za kifamasia kwa ajili ua ugonjwa wa
kisukari, yalifikia kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 3.2 mnamo mwaka 2006.
Baada ya hapo ziliibuka taarifa za kitafiti kwamba dawa hii ilikuwa inasababisha
madhara makubwa ya kiafya kwa mtumiaji kama
vile ongezeko la hatari ya shambulizi la moyo (heart attack), wepesi wa
kuvunjika mifupa na hususan ile ya mikononi juu ya kiwiko, uharibifu wa macho,
kiharusi na uharibifu wa ini kutokana na ongezeko la sumu. Inakadiriwa kuwa
ndani ya Marekani peke yake kati ya mwaka 1999 na mwaka 2006 dawa hii
ilisababisha mashambulizi ya moyo (heart attacks) na vifo kati ya 60,000 na
200,000.
Japokuwa baadhi ya matatibu wa dawa za asili na zile za tiba
mbadala wanadai kuwa wanatibu ugonjwa huu, madai haya yanapaswa kuchukuliwa kwa
tahadhari. Ni kweli kuwa mtu anaweza kuwa na dawa ya kuondoa sababu moja au
zaidi ya kisukari na hivyo kumsaidia mtumiaji kuondokana na dalili zote za
ugonjwa huo. Hata hivyo hii haina maana kwamba dawa hiyo itamtibu kila mgonjwa
wa kisukari. Kwa kifupi ni kwamba kundi la wenye kisukari kilichosababishwa na
sababu zinazoguswa na dawa husika watapona, na wengine wenye kisukari
kilichosababishwa na sababu zisozoguswa na dawa hiyo hawatapona.
Mazoea yana tabu sana.
Tulio wengi hatuli chakula kwa kuzingatia kanuni za afya bali tunakula kwa
ajili ya mazoea na kulenga ladha. Mgonjwa wa kisukari mwenye nia ya kuidhibiti
hali hiyo analazimika kuachana kabisa na kula kwa mazoea na kulenga ladha. Anatakiwa
ajue kuwa vyakula vyote vya wanga, na hususan vile vilivyochakatwa kwa kiwango
kikubwa, vina madhara makubwa kwake na anatakiwa kuviendea kwa tahadhari kubwa.
Hali hii huwa ni chanzo kikubwa cha kufadhaika kwa baadhi ya watu ambao
wamepata ugonjwa wa kisukari. Baadhi yao
huuliza kwa ghadhabu : ‘sasa utakula nini???!’ na kuendelea kula vyakula vyao
walivyozoea huku wakisaidiwa kisaikolojia na kimwili na vidonge wanavyopewa
hospitalini na madaktari wao. Waathirika wengi wa madawa kama
avandia ni wale wanaoangukia katika kundi hili.
Kisukari pia kinatisha kwa kuwa kinasababisha mololongo wa
matatizo mengine kibao ya kiafya. Matatizo haya ni pamoja na uharibifu wa macho
unaotambulishwa na magonjwa kama glaucoma
(uharibifu wa neva za jicho), cataracts (ukungu kwenye lenzi ya
jicho), retinopathy (uharibifu
mkubwa katika retina ya jicho), nakadhalika. Matatizo ya miguu yanayotambulishwa na
magonjwa kama neurapathy(maumivu yatokanayo na uharibifu wa mishipa ya
fahamu), ulcers (vidonda sugu), gangrene (mkusanyiko wa tishu
zilizokufa kutokana na kutofikiwa na mzunguko wa damu), nakadhalika. Matatizo
mengine ni yale ya magonjwa ya ngozi na magonjwa ya moyo.
Faraja ya ugonjwa wa sukari ni kuufatilia kwa makini. Hii
ina maana kuwa ni muhimu kufanya kipimo kila siku, ikiwezekana hata mara mbili
au tatu kwa siku. Kutokana na hali hii gharama za kuufuatilia ugonjwa huu ni
kubwa na huathiri kwa kiasi kikubwa hali ya kiuchumi ya mgonjwa. Kwa mfano tu,
hivi sasa katika zahanati na vituo vingi vya afya, gharama za kupima kisukari
kwa mara moja ni kati ya shilingi 2,000.00 na shilingi 2,500.00. Unapomwambia
mtu apime mara tatu kwa siku maana yake atumie kati ya shilingi 6,000 na
shilingi 7,500.00 kila siku!
Mwisho kisukari kinatisha kwa sababu taratibu kinaonekana
kunyemelea hadhi ya kuwa ni janga kubwa sana
la kijamii. Katika pande zote za dunia kisukari kinaongezeka badala ya
kupungua. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, dunia inatarajiwa kuwa na
wagonjwa wa kisukari 366,000,000 mwaka 2030 kutoka wagonjwa 171,000,000 waliokuwepo
mwaka 2,000. Hili ni ongezeko la aslimia
53! Tanzania, ambayo mwaka 2,000 ilikuwa na wagonjwa 201,600 inatarajiwa kuwa
na wagonjwa 605,000 mwaka 2030, ikiwa ni ongezeko la 66.7%
Hata hivyo janga la kisukari linaoonekana kuzikumba zaidi
zile nchi ambazo raia wao wanapendelea mno vyakula vya wanga katika mitindo
tofauti- soda, pasta, doughnut, keki, mikate, lambalamba, nakadhalika. Nchi
kama Italy
uwiano kati ya Wataliano wanaoumwa kisukari na wale ambao hawaumwi ni 1:14!. Inawezekana
sababu kubwa ikawa ni piza, pasta na spaghetti. Hivi ni vyakula
vinavyotengenezwa kwa ngano na Wataliano wanavifakamia kwa wingi.
Marekani uwiano wao ni 1:17. Hii nayo ni jamii ambayo
imelogewa soda, doughnut, chips, pizza, na vyakula vingine vya wanga vilivyochakatwa
kwa kiwango cha juu. India
uwiano wao ni 1:39. Hawa nao ni mabingwa wa vitu vitamu. Wahindi ni wafakamiaji
wa tamutamu za kila aina na sifa kuu ya tamutamu hizi ni wingi wa sukari,
ngano, mafuta na rangi.
Tanzania
ina uwiano wa 1:238. Huu ni uwiano mzuri sana
ukilinganisha na nchi tulizotangulia kuzitaja. Sababu ya uwiano huu mzuri ni
nini wakati kimsingi sehemu kubwa ya Watanzania ni wala wanga zaidi kutokana na
hali zao za kiuchumi? Nadhani sababu kubwa ni ukweli kwamba Watanzania wengi ni
wakaazi wa vijijini na kimsingi pamoja na kwamba sehemu kuwa ya chakula chao ni
wanga, lakini kutokana na sababu za kiuchumi, wanalazimika kuula wanga huo
katika mfumo ambao haujachakatwa.
Kuepukana na ugonjwa wa kisukari ni muhimu kufanya kipimo
cha kutambua aina ya mwili wako katika kuchakata vyakula (metabolic typing
test) na iwapo utagundulika kuwa wewe ni mchakataji wa protini haraka uchukue
hatua za kupunguza kwa kiwango kikubwa ulaji wa wanga, na hasa ule ambao umechakatwa
kwa kiwango kikubwa. Nafasi ya wanga (kwa ajili ya kuzalisha nishati ya
matumizi ya mwili) ichukuliwe na mafuta bora ya kula – nazi, siagi, samli,
zaituni. Nafasi ya wanga kwa ajili ya kujaza tumbo ichukuliwe na mboga
mchanganyiko za majani, na pale ambapo uwezekano upo, sehemu kubwa ya mboga
hizo iwe mbichi (salad). Mafuta ya kawaida (yale tuliyoyazoea) tunaweza
kuendelea kuyatumia (siyo kwa kupikia) bali kwa kupambia saladi (salad
dressing).
Aidha kama wewe tayari ni mgonjwa wa kisukari, utanufaika sana kwa kuondoa wanga uliochakatwa katika orodha ya
vyakula vyako na ukaingiza wanga ambao haujachakatwa, tena kwa kiwango kidogo sana kma mbadala wake. Kwa
ajili ya kuupatia mwili nishati punguzo hilo
la wanga lichukuliwe na ongezeko la mafuta bora ya kula – nazi, siagi, samli,
na zaituni. Aidha nafasi ya kushiba ichukuliwe na wingi wa mchanganyiko wa
mboga za majani, ikiwezekana sehemu kubwa ya mboga hizi iwe mbichi (salad).
Kama ilivyo kwa yule
anayelenga kukwepa kuugua kisukari, mafuta ya kawaida (yale tuliyoyazoea)
tunaweza kuendelea kuyatumia (siyo kwa kupikia) bali kwa kupambia saladi.
Ushauri huu kuhusu mafuta ni kinyume kabisa na ushauri mnaopatiwa na madaktari
wenu kuhusu mafuta ya kula. Hata hivyo kisayansi ndio ushauri sahihi. Mungu
akipenda post yetu ijayo itazungumzia jambo hili kwa kina ili kuliweka katika
mazingira ya kueleweka zaidi..






No comments:
Post a Comment