Kisukari
cha ukubwani ni nini?
Kisukari
cha ukubwani ni hali inayojitokeza pale mwili wako unaposhindwa kuchakata
sukari aina ya glucose na hivyo kuifanya ilundikane kwenye damu, badala ya
kwenda katika seli za mwili ili itumike kuzalisha nishati ya kuendeshea
shughuli za mwili. Mlundikano huu wa sukari kwenye damu una madhara mengi sana
kiafya, kiasi kwamba hatua zisipochukuliwa kuondoa mlundikano huo kwenye damu,
madhara hayo yanaweza kuishia kusababisha magonjwa hatari yanayoweza kupelekea
kwenye ulemavu na kifo.
Magonjwa
yenye uhusiano na mlundikano wa sukari kwenye damu ni yapi?
Baadhi ya
magonjwa yenye uhusiano na mlundikano wa sukari kwenye damu ni shinikizo la juu
la damu (hypertension), ugonjwa wa moyo, ugonjwa wa figo, ugonjwa wa ini,
uharibifu wa mishipa ya damu na ile ya fahamu, uharibifu wa macho, uharibifu wa
ubongo, na maambukizi ya mara kwa mara ya vimelea vibaya vya maradhi hasa
tumboni na kwenye njia ya haja ndogo. Aidha ni rahisi kwa mtu anayekabiliwa na
mlundikano wa sukari kwenye damu kushindwa kupona majeraha na hivyo kuwa katika
hatari ya kupoteza viungo vya mwili, ikiwa ni pamoja na kupata upofu.
Sababu za
kisukari cha ukubwani
Sababu za
kisukari cha ukubwani ziko nyingi. Hapa tutazungumzia moja nayo ni kiungo
kinachoitwa kongosho kushindwa kuzalisha homoni ya insulin ya kutosha. Insulin
ndiyo homoni inayofanya kazi ya kubeba sukari na kuisafirisha kutoka kwenye
damu na kuiingiza katika seli za mwili. Hii insulin inazalishwa na kundi la seli
zinazopatikana kwenye kongosho zinazoitwa beta. Seli hizo zinaposhindwa kufanya
kazi kwa sababu moja au nyingine kiasi cha isulin kinachozalishwa hupungua sana
na hivyo kusababisha sukari ianze kulundikana kwenye damu.
Uharibifu
wa kongosho.
Kumefanyika
tafiti nyingi zilizolenga kubaini chanzo cha seli za beta kushindwa kazi.
Baadhi ya hizi tafiti zimebaini kuwa maambukizi katika kongosho, hususan
yanayotokana na virusi yanaweza yakaharibu seli hizi na hivyo zikaacha kufanya
kazi. Hata hivyo tafiti nyingi zimebaini kuwa sababu kubwa ni uchovu. Tafiti
hizi zimebaini kuwa kutokana na ulaji wa wanga uliopitiliza mipaka, hasa ule
uliochakatwa (wali mweupe, sembe, chapati, mikate, chips, keki, sukari, soda,
nakadhalika), seli hizi hupambana kuzalisha insulin ya kuondoa mzigo wa sukari
unaoingia mwilini kila mara kupitia vyakula hivi, lakini hatimaye huzidiwa
nguvu na kunyoosha mikono!
Kongosho
linaweza kutibika!
Bahati
nzuri tafiti zimebaini pia kuwa kisukari kinachokuja kutokana na mazingira haya
kinaisha iwapo seli za beta zitapewa muda wa kutosha kupumzika. Imebainika kuwa
seli hizi huanza tena kuzalisha insulin ya kutosha pale uchovu ziliokuwa nao
unapomalizika. Ili kuzipumzisha seli zako za beta kuna haja ya kuondoa kabisa
vyakula vinavyozalisha glucose kweye lishe yako. Miongoni mwa hivi ni hivyo
tulivyotangulia kuvitaja katika paragraph iliyotangulia. Ili kupata nishati ya
kutosha katika kipindi hiki utahitajika kuongeza kiasi cha mafuta bora ya kula
kwenye kila mlo wako. Kumbuka mafuta bora zaidi ni yale ambayo ni koza
(saturated fats) ikiwa ni pamoja na nazi, mafuta ya zaituni (olive oil), na
siagi (butter). Mafuta ambayo siyo koza (polyunsaturated fats) kama yale ya
alizeti yanaweza kufaa pia alimradi tu iwapo yataliwa katika hali ya ubichi.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba mafuta haya yanapopikia hubadilika na
kutengeneza mafuta tenge (trans fats) ambayo tafiti zimebaini kuwa yanapoingia
mwilini hulundikana kwenye mishipa ya damu na kuwa chanzo cha uharibifu mkubwa
kwenye mfumo wa mzunguko wa damu.
Muda wa
kusubiri
Swali ni
je, seli za beta hupumzika kwa muda gani kabla ya kuanza kufanya tena kazi?
Muda wa haya mapumziko utatofautiana kati ya mtu na mtu kulingana na muda
aliodumu na sukari yake kabla ya kuchukua hatua za kupumzisha hizo seli. Kwa
bahati mbaya watu wengi huishi na mlundikano wa sukari kwenye damu kwa muda
mrefu kabla ya kubainika kuwa ana tatizo hilo. Hii ni kutokana na ukweli kuwa
baadhi ya dalili za kuwepo kwa sukari nyingi kwenye damu zinaweza pia
zikasababishwa na magonjwa mengine. Kwa bahati mbaya ni madaktari wachache
wanaokumbuka kuwapima wagonjwa wao kisukari pale wanakutana nao. Hii inaweza
ikapelekea mtu kuishi na kisukari muda mrefu sana kabla ya hatimaye kugunduliwa
kuwa anacho.
Chukua
hatua
Jambo la
msingi ni kwamba kama unataka kuzuia usipate tatizo la kisukari au unataka
tatizo hilo liondoke mapema kadri iwezekanvyo baada ya kubainika, basi
unalazimika kuchukua hatua stahiki. Hatua hizi ni pamoja na:
1.
Kupunguza sana ulaji wa vyakula tulivyotaja hapo juu. Hatua hii itakusaidia
kujikinga na tatizo la kisukari katika maisha yako yote.
2. Kama
huwezi kupunguza vyakula tulivyovitaja hapo juu, basi jitahidi kupima sukari
walau mara moja kila baada ya majuma mawili. Hatua hii itakusaidia kugundua
mapema kuwa tayari umeshapata tatizo na itakusaidia kuchukua hatua mapema za
kuacha kula vyakula ambavyo vinalisumu kongosho lako. Kadri unavyochukua hatua
mapema ndivyo itakavyokuwa rahisi kwa seli za beta katika kongosho lako kurejea
katika hali yake ya kawaida.
3. Kama
wewe tayari ni mgonjwa wa kisukari cha ukubwani na unataka upone na kuachana na
matumizi ya kila siku ya dawa (ambazo aghalabu huwa na athari mbaya za
pembeni), basi achana na ulaji wa vyakula tulivyotaja hapo juu. Hatua hii
itaanzisha mchakato wa kupumzisha seli za beta za kongosho lako na kama
zilikuwa hazijaharibika kabisa, baada ya muda zitarejea katika kufanya kazi
kama kawaida.
Sasa tule
nini?
Wagonjwa
wengi wenye kisukari huishi maisha magumu sana, pale wanapotaka kuchukua hatua
kuondokana na kisukari chao kwa njia ya kubadilisha lishe, hususan wanapokuwa
mbali na makaazi yao. Tatizo ni kwamba jamii haijui kabisa kuwa ugonjwa wa
sukari hivi sasa ni tatizo kubwa na kwa hivyo migahawa mingi haijaweka kabisa
mazingira ya kuweza kuwahudumia watu wenye kisukari. Hata hivyo kama unajua
aina ya chakula unachopaswa kula unaweza ukachukua hatua ya kuzungumza na hao
wenye migahawa na walio wengi wako tayari kukusaidia.
Kwa
ujumla mtu anayetaka kuachana na kisukari alichonacho anapaswa kula aina ya
lishe inayoitwa ketogenic. Hii ni lishe ambayo hujumuisha protini kidogo, kiasi
kikubwa cha mchanganyiko wa mboga za majani, na kiasi cha kutosha cha mafuta
koza.
Protini
kidogo tu yatosha!
Ni muhimu
kuzingatia kuwa mwili hauhitaji protini nyingi. Kiasi kingi cha protini kina
madhara kiafya kutokana na chakula hiki kuzalisha kiasi kikubwa sana cha
tindikali ndani ya mwili. Baadhi ya taifiti zimeonyesha kuwa kiasi cha gramu 27
tu za protini kwa siku zinatosha. Hawa wanadai kuwa kuasi cha protini
kinapozidi hapo mzigo wa tindikali mwilini unakuwa ni mkubwa mno kiasi kwamba
mifupa ya mwili inaanza kuachia madini ya kalisi (calcium) kuingia katika
mzunguko wa damu ili kusaidia kuzimua hiyo tindikali. Hata hivyo kundi kubwa la
watafiti hupendekeza kati ya gramu 50 na 70 tu kwa siku. Vyakula vya protini ni
pamoja na nyama (aina zote), maziwa, mayai, samaki, na wadudu kama senene,
nakadhalika. Kuna baadhi ya vyakula ambavyo asili yake ni mimea ambavyo vimebea
pia kiasi kikubwa sana cha protini. Hivi ni vile vya jamii ya kunde mathalani
soya, maharage, kunde zenyewe, njegere, nakadhalika.
Sasa nitembee na mzani?
Ukweli wa mambo ni kwamba huhitaji kutembea na mzani.
Hakikisha tu kwamba kiasi cha 80% ya nafasi katika sahani yako ya chakula
kimechukuliwa na mchanganyiko wa mboga za majani, ikiwezekana 50% - 75% ya hizo
mboga ziwe katika hali ya ubichi (vegetable salad). Katika ile 20% ya nafasi
iliyobaki nusu inaweza kuchukuliwa na chakula cha protini chochote na nusu
inaweza kuchukuliwa na mafuta koza yoyote uliyonayo.






No comments:
Post a Comment