Friday, June 10, 2016
KISUKARI CHA UKUBWANI KINAWEZA KUTIBIKA
KISUKARI CHA UKUBWANI – KANUNI YA MSINGI KATIKA KUJITIBU!
Kanuni ya msingi katika kujitibu kisukari cha ukubwani ni kufanya jitihada kudhibiti kiwango cha sukari kwenye mzunguko wa damu kibaki ndani ya wigo unaokubalika kwa kadri inavyowezekana. Sambamba na hilo jitihada zifanyike pia kuzuia uharibifu wa viungo muhimu vya mwili unaosababishwa na wingi wa sukari kwenye mzunguko.
Sukari ya ziada kwenye mzunguko wa damu husababisha madhara hata kwa wale ambao bado hawajapata ugonjwa wa kisukari. Sukari huongeza kasi ya kuzeeka kutokana na kuungana na protini za mwili kuzalisha kampaundi (compounds) zinazoitwa Advanced Glycation End Products, au kwa kifupi AGES. AGES husababisha protini husika kupoteza unyumbufu (supponess) na kukakamaa, pamoja na kukumbwa na mfuro (inflammation). Mchakato wa kuzalisha AGES huitwa glycosylation au glycation. Kadri kiwango cha sukari kwenye mzunguko wa damu kinavyokuwa kikubwa ndivyo mchakato huu unavyofanya kazi kwa haraka na kupelekea madhara yake kujidhihirisha.
Aghalabu AGES husababisha madhara makubwa ndani ya mwili. Mfuro uliosababishwa na Mchakato wa Glycosylation ni chanzo cha matatizo luluki ya kiafya ndani ya mwili. Ugonjwa wa moyo, shinikizo la damu, upofu, uharibifu wa figo na majeraha yasiyopona ni miongoni mwa madhara yanayoweza kusababishwa na huu Mchakato wa Glycosylation.
Moja ya protini zinazoathiriwa sana na sukari mwilini ni ile inayojulikana kama collagen. Collagen ni protini ambayo inatumika kama malighafi kwa ajili ya kuundia tishu maalum zinazotimika kama kiungo au daraja baina ya tishu mbalimbali mwilini. Kitaalamu hizi tishu hujulikana kama connective tissues. Protini hii inapopata mfuro na kupoteza unyumbufu kutokana na sukari hupelekea tishu zinazoundwa nayo (connective tissues) kupungukiwa na uwezo wake wa kushikilia tishu nyingine.
Hali hii huathiri uimara na utendaji wa viungo mbalimbali vya mwili kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano, mishipa ya damu ambayo kwa kiasi kikubwa imeundwa na collagen hupata mkakamo, na mkakamo huo huzaa ongezeko la shinikizo la damu na kusababisha msongo (stress) mkubwa kwa moyo. Msongo huu husababisha uharibifu wa misuli na mishipa ya moyo na hatimaye kuzalisha magonjwa mbalimbali ya moyo.
Mchakato wa Glycosylation ni tatizo kubwa kwa wenye ugonjwa wa kisukari. Mchakato huu ndiyo sababu kuu ya madhara yote ya muda mrefu yanayowakumba wagonjwa wa kisukari. Hii ni kwa sababu mchakato huu hutokea kwa kasi kubwa zaidi na kwa nguvu kubwa zaidi kwa wagonjwa wa kisukari kuliko wale ambao siyo wagonjwa.
Ukiondoa kusababisha Mchakato wa Glycosylation, sukari ya ziada kwenye damu pia huharibu mfumo wa mishipa ya fahamu, hususan ile iliyoko nje ya ubongo, uti wa mgongo na katika kivunge cha mishipa ya fahamu ijulikanayo kitaalamu kama ganglia. Sehemu ya mfumo wa mishipa ya fahamu inayoathiriwa na sukari kitaalamu huitwa peripheral nervous system. Uharibifu huu na ule wa mishipa ya damu kwa pamoja husababisha tatizo la gangrene, yaani kufa kwa kiasi kikubwa cha tishu, hususan katika baadhi maeneo ya miguuni. Macho na figo pia huathiriwa kwa kiasi kikubwa na huu uharibifu.
Tatizo lingine linalosababishwa na ulaji wa sukari na wanga ni ongezeko kubwa la ghafla la sukari kwenye mzunguko wa damu baada tu ya kumaliza kula. Kitaalamu ongezeko hili huitwa postprandial hyperglycemia. Tafiti zimethibitisha kuwa ongezeko hili la ghafla la sukari huharibu kuta za ndani za mishipa ya damu. Ili kuzuia hii hali baadhi ya madaktari hupendekeza matumizi ya dawa fulani fulani za kuzuia sukari kuingia kwenye damu kabla ya kula.
Utaratibu huu unashangaza sana. Haiingii akilini ni kwa nini mtu abugie sukari na wanga, kisha anywe dawa kuzuia asije akawa na ongezeko kubwa la sukari kwenye damu ambalo litamsababishia madhara. Ukweli wa mambo ni kwamba mgonjwa wa kisukari cha ukubwani akipunguza kula sukari na wanga baada ya muda fulani hahitaji kutumia tena dawa ya aina yoyote ile. Mgonjwa wa kisukari hatakiwi kupata hofu yoyote juu ya hili kwa sababu katika makundi yote makuu ya chakula, ni sukari na wanga pekee visivyo na ulazima kwa ajili ya kufanya maisha yadumu na kuendelea.
Wataalamu wa tiba za kisukari zisizokwenda sambamba na matumizi ya dawa za kifamasia wanasema hatua ya kwanza ni kupunguza kiasi cha wanga katika lishe. Kiasi cha gramu 60 za wanga au chini kidogo kwa siku kinapendekezwa.
Hatua ya pili ni kuzingatia ubora wa chakula. Chakula kinatakiwa kiwe kimejaza idadi kubwa ya viini-lishe kadri inavyowezekana. Hii ni kwa sababu baadhi ya hivi viini-lishe hutoa ulinzi dhidi ya uharibifu unaosababishwa na sukari. Nchi nyingi za bara la Asia zina historia ndefu ya kutibu kisukari kwa kutumia lishe. Kwa mfano, viungo vingi vinavyotiwa kwenye chakula nchini China huzuia ongezeko la sukari kwenye damu. Japokuwa huko nyuma watu walijifunza jinsi ya kutumia viungo hivi bila kujua jinsi vinavyofanya kazi ndani ya mwili, leo inafahamika kuwa viini-lishe vilivyoko katika hivi viungo hufanya kazi kwa kuzuia utendaji kazi wa kimeng’enya kinachoitwa alpha glucosidase. Moja ya majukumu ya kimeng’enya hiki ni kuchakata wanga na kuubadili kuwa sukari nyepesi ya glucose. Glucose ndiyo sukari inayolundikana kwenye damu baada ya kula sukari ya kawaida na wanga.
Viini-lishe vinavyozuia utendaji kazi wa alpha glucosidase kwa kawaida huzuia ongezeko la ghafla la sukari kwenye damu, yaani postprandial plasma glucose. Kwa wagonjwa wa kisukari cha ukubwani viini-lishe hivi hupunguza ongezeko la sukari kwa kiasi cha 40 - 50 mg/dL (2.2 - 2.8 nmol). Miongoni mwa viini-lishe vinavyozuia utendaji kazi wa alpha glucosidase ni pamoja na vile vinavyojulikana kitaalamu kama anthocyanins, polyphenols, flavonoids, terpenoids na, curcuminoids. Hii ina maana kuwa viungo vingi, kwa mfano mdalasini, binzari nyembamba (jira), tangawizi, manjano, uwatu, na kalonji (black seed); mboga takriban zote za majani; mboga za jamii ya kunde; na matunda kama maboga, parachichi, zambarau, karela (bitter gourd), papai, tikiti maji na nazi ni msaada mkubwa kwa wagonjwa wa kisukari, na wale wanaotaka kujikinga wasipate kisukari hicho.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)






No comments:
Post a Comment