Friday, June 10, 2016

KISUKARI CHA UKUBWANI KINAWEZA KUTIBIKA - HAKIKISHA MWILI WAKO HAUNA MLUNDIKANO WA TINDIKALI




Mwili wako umejaa tindikali?

Moja ya sababu kubwa za kisukari cha ukubwani ni mwili kujaa tindikali.

Tindikali ni nini?

Tindikali ni kitu chochote ambacho kinaongeza wingi wa atomu za hewa ya hydrogen zilizobeba umeme chanya [hydrogen ions (H+)] katika kimiminika chochote.  Atomu ni kipande kidogo kuliko vyote katika kiasili (chemical element) fulani cha kikemia ambacho hakijapoteza tabia za kikemikali za kiasili hicho.
Uzimuaji wa tindikali

Kitu chochote chenye uwezo wa kuzimua tindikali, kwa maana ya kupunguza idadi au kuondoa  kabisa kiasi cha wa atomu za hewa ya hydrogen zilizobeba umeme chanya, kinaitwa alkali. Kwa kawaida alkali mbalimbali huwa zinasababisha kupatikana kwa chembechembe za kikemia zilizobeba umeme hasi zinazoitwa [hydroxl ions (OH-)] pale alkali hiyo inapochanganywa na maji.  

Je, kitu hiki ni tindikali au ni alkali?

Kipimo cha kupima udhaifu au ukali wa kitu kwa munasibu wa utindikali au ualkali wake kwa kitaalamu kinaitwa pH. Herufi hizi ni kifupi cha ‘potential of Hydrogen’, ikiwa na maana ya ‘wingi wa hydrogen’. Mzani wa kupimia pH ya kitu chochote umegawanywa katika vipimo vidogo vyenye tarakimu kuanzia 0.00 hadi 14.00. Nambari 7.00 inawakilisha pH ya kitu chochote kilichozimuliwa (neutral). Tarakimu yoyote chini ya nambari 7.00 na kushuka hadi 0.00 inawakilisha utindikali wa kitu na tarakimu yoyote juu ya nambari 7.00 na kupanda hadi 14.00 inawakilisha ualkali wa kitu.

Kadri nambari inavyozidi kuwa ndogo kutoka 7.00 ndivyo ukali wa tindikali unavyozidi na kadri nambari inavyozidi kuwa kubwa kutoka katika 7.00 ndivyo ukali wa alkali unavyozidi.

Asili ya maumbile yetu

Katika maumbile ya asili ya mwanadamu, sehemu pekee yenye vimiminika vyenye tabia ya tindikali ni kwenye mfuko wa tumbo. pH ya kwenye mfuko wa tumbo ni kati ya 1 -3, lakini mara nyingi inakaribiana zaidi na 2.  Hii inaonyesha kuwa tindikali iliyoko tumboni ni kali sana!

Tunapozungumzia vimiminika mbalimbali yaliyoko mwilini, kuna haja ya kupima pH kwa ukamilifu zaidi na siyo kwa tarakimu nzima. Hii ni kutokana na ukweli kuwa katika ‘ulimwengu wa pH’ kuna tofauti kubwa sana kati ya tarakimu mbili nzima zinazofuatana. Kwa mfano pH ya 5.0 inaonyesha utindikali wenye ukali mara kumi zaidi kuliko pH ya 6.0, lakni pH ya 4.0 inaonyesha utindikali wenye ukali mara mia zaidi (10 x 10) kuliko pH ya 6.0! Hivyo basi mabadiliko kidogo sana katika pH mwilini yanawakilisha mabadiliko makubwa sana katika jinsi ambavyo mwli wako unafanya kazi.

Kwa kawaida pH  ya vimiminika mbalimbali mwilini mwako hubadilika badilika kulingana na kile kinachoendelea ndani ya mwili. Iwapo mabadilko katika pH yatakuwa makubwa sana au yatakuwa endelevu, basi mwili wako utakumbana na matatizo ya kiafya.

Vimiminika vilivyoko ndani ya mwili

Kuna vimiminika vya aina nyingi sana mwilini. Mwili wa mtu mzima mwenye umbo la wastani unabeba kiasi cha lita 40 za majimaji ya aina mbalimbali – damu, mate, nyongo, mkojo, ‘juisi’ za kongosho, nakadhalika. Kuna vimiminika ndani ya seli na nje ya seli, kama sehemu ya damu, kuzunguka viungio, ndani na kuuzunguka ubongo pamoja na uti wa mgongo, ndani ya viungo (organs) na kuvizunguka.

Kwa mujibu wa rejea mbalimbali za kitabibu, majimaji haya yote ukiondoa yale yaliyoko kwenye mfuko wa tumbo yana au yanaweza kuwa na ualkali, yaani kuwa na pH zaidi ya 7.0.   Vifuatavyo ni viwango vya pH vya vimiminika mbalimbali vinavyokubaliwa kitabibu kuwa ni vya kawaida.
      Damu………………………………………………………………  7.35 -7.45
      Vimiminika vya uti wa mgongo (spinal fluid)……………………    7.30 – 7.50
      Mate (saliva)………………………………………………………   6.50 -  7.50
      Vimiminika vya tumboni (gastric fluids)………………………        1.00 – 3.00
      Vimiminika vya utumbo mwembamba (duodenum)…………….     4.20 – 8.20
      Haja Kubwa (feses)…………………………………………………            4.60 – 8.40
      Mkojo (urine)………………………………………………………  4.80 – 8.40
      Kongosho (pancreas)………………………………………………  8.00 – 8.30
      Nyongo iliyozalishwa na ini (Liver bile)……………………………7.10 – 8.50
      Nyongo iliyohifadhiliwa kwenye kifuko cha nyongo (Gall Bladder Bile)………………………………………………………...........     5.50 – 7.70
           
Kwa kutazama jedwali hilo hapo juu utaona kuwa vimiminika vyote mwilini ukiondoa vile vya mfuko wa tumbo vinapaswa kuwa na ualkali, yaani vikipimwa, kipimo cha pH kitasoma juu ya 7.00. Kama hali ndiyo hii, ni kwa nini basi baadhi ya viungo nyeti sana, katika hali halisi, vinakuwa vimebeba au vinazalisha vitu vyenye utindikali wa hali ya juu?

Ni rahisi kuelewa ni kwa nini vimiminika vya mfuko wa tumbo vina utindikali mkali (pH ya kati ya 1.00 na 3.00). Vimiminika hivi vina kazi kubwa ya kulainisha ‘vitu vigumu’ (vyakula) kama moja ya hatua za awali  za kuchuja na kufyonza virutubisho kwa ajili ya matumizi ya mwili.   Lakini kwa nini kuwe na kutofautiana sana katika upeo wa pH kwa baadhi vimiminika ndani ya mwili, hususan vile ambavyo kimsingi vinapaswa kuondolewa mwilini mara kwa mara, mathalani mkojo na kinyesi? Ni kitu gani kinaweza kusababisha mkojo uwe na upeo wa pH ya 4.8 inayoashiria utindikali mkali na wakati mwingine pH ya 8.4 inayoashiria ualkali wa wastani? Lakini lililo muhimu zaidi ni kujiuliza: Ni kitu gani kinasababisha kupanda huku na kushuka kwa pH (fluctuation), kuwe ni kwa lazima? 

Mchango wa Lishe, Msongo na Mchakato wa Kawaida wa Kuishi

pH  haiwezi kubadilika bila kuwa na kichocheo (stimulus). Aghalabu kichochocheo huwa ni kitu tulichokula au msongo (stress), na kwa kiasi fulani mchakato wa kawaida wa kuishi. 

Lishe

Japokuwa vyakula vingi si tindikali pale vinapoingia kwenye vinywa vyetu, jivu la vyakula hivyo linalobaki baada ya mchakato wa kutoa nishati iliyomo kwenye vyakula hivyo kwa ajili ya matumizi ya mwili, ni lenye asili ya utindikali. Utindikali huu huathiri pH ya vimiminika vilivyoko mwilini ambayo huanza kushuka. Kama chakula unachokula kinaacha jivu la tindikali kali, ni suala la muda tu kabla ya vimiminika vya seli za mwili wa wako na vile vilivyomo kwenye mazingira ya nje ya seli kuelemewa na tindikali hiyo.

Msongo

Hali ni hiyo hiyo unapokabiliwa na msongo. Msongo ni kitu kinachounguza nishati nyingi sana ya mwili pamoja na kuchochea mabadiliko mengine mengi katika mchakato wa uvunjifu na ujenzi wa kemikali mwilini (metabolic processes). Vitendo hivi huzalisha tindikali nyingi ndani ya mwili ambayo pia huchangia pH ya vimiminika vilivyoko mwilini kushuka.

Mchakato wa Kawaida wa Kuishi

Shughuli mbalimbali za viungo vya mwili hutumia nishati. Matumizi haya ya nishati huzaa hewa ukaa (carbon dioxide). Hewa ukaa inapochanganyika na majimaji huzaa tindikali dhaifu ya carbon (carbonic acid). Pamoja na udhaifu wake tindikali ya carbon nayo pia inauwezo wa kuchangia pH ya vimiminika vilivyoko mwilini kushuka.

Mwili unajiteteaje?

Kama tulivyokwisha ona, asili ya vimiminika vingi ndani ya mwili ni kuwa katika hali ya ualkali.  Kwa sababu hii mwili una mifumo ya kujaribu kuondoa tindikali inayozalishwa mwilini ili isije ikabadili mazingira haya. Kuna mifumo mikuu miwili inayotumika kufanya kazi hii. Mfumo wa kwanza ni ule wa njia ya haja (hususan haja ndogo). Mara nyingi jivu la tindikali linalotokana na chakula, na tindikali inayozalishwa mwilini kutokana na msongo, huondolewa kwa njia hii. Kabla ya tindikali hii kutolewa mwilini huzimuliwa kwanza na madini ya alkali yaliyoko katika mfumo wa kiorganic (yalitokana na viumbe hai) ambayo yako mwilini kutokana na vyakula tunavyokula vyenye madini hayo, yaani matunda na mboga mboga za majani. 

Mfumo wa pili ni ule unaohusisha kupumua. Kupitia kupumua, tindikali dhaifu ya hewa ukaa inayotokana na utendaji wa kila siku wa viungo vya mwili  hutolewa nje.
Athari za upungufu wa madini ya alkali

Kutokana na watu kutozingatia kanuni za lishe sehemu kubwa ya lishe yao ni ile inayozalisha jivu jingi la tindikali ndani ya mwili. Hali hii hupelekea kupungua sana na hata kwisha kwa kiasi cha madini ya alkali yaliyoko mwilini. Hali hii ikitokea tindikali iliyoko mwilini inaweza ikaunguza vibaya sana njia ya mkojo wakati wa kuitoa. Ili hili lisitokee mwili ’huwasha’ mifumo ya dharura (backup systems) ya kuizimulia hiyo tindikali. 

Awali mwili kwa kutumia chembechembe za kiasili cha Nitrogen zilizoko mwilini (kutoka kwenye vyakula vya protini), utazalisha gesi ya Ammonia. Gesi hii ina ualkali wa hali ya juu na itatumika kuzimulia tindikali kabla ya kutolewa nje na mkojo. Hii ndiyo sababu kuna wakati mtu unakojoa mkojo wenye kutoa harufu kali ya kukereketa. Mkojo unakuwa umechanganyika na kiasi kikubwa cha ammonia na ammonia ni yenye harufu kali ya kukereketa.

Mfumo wa pili wa dharura ni ule unaotumia madini ya kalisi (calcium) kutoka katika mifupa. Iwapo pamoja na mwili kuzalisha ammonia ili kuzimua tindikali bado tindikali hiyo itaendelea kuwa nyingi ndani ya mwili, basi mwili huwasha mfumo wa pili wa dharura, ambao ni ule unaohusisha madini ya kalisi kuyeyuka kutoka katika mifupa na kuingia katika mzunguko wa damu ili yatumike kuzimulia hiyo tindikali.

Uwashaji wa mifumo hii ya dharura ni katika jitihada za mwili kuhakikisha kuwa upeo (range) wa pH ndani ya seli za mwili unabaki kuwa mdogo kadri inavyowezekana. Ili haya yawezekane baadhi ya viungo vya mwili hulazimika kufanya marekebisho ya jinsi vinavyofanya kazi. Kwa bahati mbaya marekebisho haya yanapokuwa ni ya kudumu hubadili utendaji wa mifumo ya mwili, na mabadiliko haya yanaweza yakazaa maradhi mbalimbali.
.  
Je, ni upi uhusiano kati ugonjwa wa kisukari na mlundikano wa tindikali mwilini?

Kama tulivyokwisha ona, mzigo wa tindikali unaotokana na vyakula (hususan vile vya jamii ya protini na wanga) ni lazima uzimuliwe kabla ya kutolewa nje ya mwili. Sehemu kubwa ya mfumo wa uzimuaji wa hii tindikali ni ule unaohusisha magadi (sodium bicarbonate) yanayozalishwa na kongosho. Kama mwili una madini ya sodium ya kiorganic ya kutosha kutokana na lishe, malighafi ya kuzalisha magadi mwilini ni ya kutosha na kongosho litafanya kazi yake kwa ufanisi.

Inapotokea kuwa malighafi ya kuzalishia magadi haitoshi, hali ya tindikali huanza kulemea viungo mbalimbali vya mwili, ikiwa ni pamoja na kongosho lenyewe. Kongosho ambalo kwa kawaida linatakiwa lifanye kazi katika mazingira yenye pH ya 8.0 – 8.30 hushindwa kufanya kazi kwa ufanisi kwa sababu pH ya mazingira yake imeshuka. Kinachofuatia ni kwamba majukumu muhimu ya kongosho yanaathirika, ikiwa ni pamoja na uzalishaji wa hormone ya Insulin ambayo ni muhimu katika uchakataji wa sukari ya kwenye damu.
Chukua hatua kukwepa janga la tindikali.

Moja ya hatua muhimu na isiyokwepeka unapotaka kuondokana na mzigo wa tindikali ndani ya mwili ni kurekebisha lishe yako. Ni muhimu kuzingatia kuwa katika makundi makuu ya vyakula, PROTINI NA WANGA huzalisha jivu la tindikali ndani ya mwili, na MBOGA ZA MAJANI NA MATUNDA (ukiondoa matunda aina ya creanberry) huzalisha jivu la alkali ndani ya mwili. Ni vizuri pia kuzingatia kuwa uwiano mzuri wa vyakula hivi kwenye mlo ni 80% MAJANI NA MATUNDA/20 PROTINI NA WANGA NA MAFUTA. KOZA.

Kurekebisha lishe yako na kuiweka katika uwiano huu ni hatua muhimu sana katika kutibu kongosho lako na hatimaye kuondokana na kisukari chako cha ukubwani.



No comments:

Post a Comment