Wednesday, June 8, 2016

NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA: SWALA, FUNGA NA SADAKA




NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA

Ibada ni mjumuiko wa mambo mengi. Kufupisha mambo tunaweza tukasema kuwa ibada ni ile hali ya kutekeleza kwa hiari maamrisho ya Mungu Muumba. Maamrisho haya yana sura mbili. Sura hizi ni: Mambo uliyoagizwa kufanya kwa upande mmoja, na kwa upande wa pili mambo ilioagizwa kuacha. Kuna faida nyingi sana ambazo mtu aliyezama kwenye ibada anazipata kiafya. Hebu kwanza tuangalie ibada katika sura ya yale ambayo Muumba ametuagiza kufanya.

1. Swala/Sala.
Swala/Sala ni kindendo ambacho kinafungua mawasiliano ya moja kwa moja baina ya mja na muumba wake. Kupitia kitendo hiki mja huelezea shida zake na kutuma maombi yake kwa yule mwenye ufunguo wa ufumbuzi wa kila jambo. Swala/sala iliyoswaliwa kama inavyopasa humuacha mja akiwa na amani na utulivu wa hali ya juu katika nafsi yake. Amani na utulivu huu huzaa faida moja kubwa sana kiafya ambayo yule ambaye hakupata swala/sala hiyo bila shaka atakuwa ameikosa.

Faida yenyewe ni kwamba mwili unazalisha homoni (hormone) inayoitwa oxytocin. Hii ni homoni ambayo ina orodha ya mambo mengi sana yenye manufaa kiafya. Baadhi ya mambo haya ni pamoja na:

(a) Inausaidia mwili kupanua mishipa ya damu na hivyo kushusha shinikizo la damu;

(b) Inapanua mishipa ya damu kwenye vifua na nyuso za kina mama wanaonyesha na kina baba waliowashika watoto wao wanaonyonya, kitendo kinachosaidia kuzalisha joto la ziada la mwili ili kuhamishia joto hilo kwa watoto hao;

(c) Inasaidia katika usagaji wa chakula pale tumbo linapokuwa limeshiba, lakini hupunguza kasi ya usagaji huo pale tumbo linapokuwa wazi;

(d) Inapunguza wingi wa homoni za msongo (stress hormones);

(e) Inatartibu uwiano wa aina mbalimbali za majimaji mwilini;

(f) Inaboresha mchakato wa kugawanyika kwa seli za mwili; na

(g) Inaharakisha kupona kwa majeraha.

Aidha tafiti zimeonyesha kuwa homoni hii inapodungwa kwa wanyama kwa njia ya sindano inapelekea wanyama hao kuwa na tabia zifuatazo:

(a) Kupunguza ukali na ukorofi na kupenda kuishi katika mazingira yenye mawasiliano ya kijamii zaidi;

(b) Kupungua kwa muda wa wanyama hao kuwa na haja ya kukutana kimwili;

(c) Kuongezeka kwa wingi wa kushika mimba, hali inayodhaniwa kuletwa na kuongezeka kwa kasi ya mbegu za dume kulekea liliko yai la jike baada ya kujamiiana.

Aidha majaribio hayo pia yalibainisha kuwa homoni hii ilisababisha panya wa kike kuonyesha tabia za ‘kimama’ hata pale ambapo panya husika walikuwa hawajawahi kuzaa hata mara moja. Mwisho ilibainika kuwa homoni hii inaweza kuwasaidia wanyama kutoathiriwa kwa kiwango kikubwa na maumivu na pia kuwa na kumbukumbu zaidi.

Swala/sala pia inaweza kuzalisha faida za ziada kutegemea na ilivyoswaliwa. Kama ni swala ya dini ya Kiislamu itakuwa inaswaliwa ikiambatana na mwondoko (movement) wa viungo. Mwondoko huu ni aina ya mazozi ya viungo ambayo humsaidia sana huyo anayeswali. Faida anazopata ni hizi zifuatazo:

(a) Mwili wake huzalisha homoni za serotonin na endorphins. Hizi zinamfanya mhusika ajisikie raha, asiathiriwe sana na vichocheo vya msongo (stress) na pia athiathiriwe sana na hisia za maumivu; na

(b) Kupungua kiwango cha uvimbe mwako (inflammation) katika seli za mwili. Matatizo ya kiafya yanayohusishwa na uvimbe mwako ni mengi mno. Mungu akipenda haya yatazungumzwa katika mada tofauti siku nyingine.

2. Funga (Swaumu)
Kufunga kula kwa muda fulani ni kitendo kingine cha kiibada chenye faida kubwa kiafya. Mtu anapokaa bila kula kwa masaa nane au zaidi hupelekea:

(a) Mafuta yaliyohifadhiwa mwilini mwake yaanze kuungua ili kuzalisha nishati ya kumsadia mhusika kuendelea na shughuli zake (Thermogenesis);

(b) Mwili huzalisha homoni ya Ghrelin ambayo bila ya kuwepo ubongo hauwezi kutengeneza seli mpya kuchukua nafasi ya zile zilizokufa au kuharibika. Homoni hii pia husaidia kufifisha athari za homini zinazochochea msongo na kukuongezea utulivu;

(c) Mwili huzalisha kiasi kikubwa zaidi cha homoni ya makuzi (human growth hormon) ambayo ni muhimu katika kujenga misuli ya mwili na ukarabati wa seli chakavu za mwili; na

(d) Mwili kuzalisha homoni ya oxytocin kutokana na amani na utulivu unaokuja kama matokeo ya funga hiyo iwapo ilikusudiwa kiroho.

3. Kutoa sadaka
Sadaka ni kitu chochote kile kiwe kinachoshikika au ni kitendo ambacho kinapelekea yule anayekipokea/kulengwa kupata nafuu fulani. Sadaka yaweza kuwa salamu tu iliyotolewa kwa bashasha, na hata tabasamu la kupendeza. Sadaka pia yaweza kuwa ni kitendo cha kumgusa mtu kwa nia ya kumfariji, au kumfanya tu ajisikie raha. Mfano wa hili ni pale unapomshika mtoto kichwani na kuchezesha chezesha kiganja chako kwenye nywele zake.

Kama sadaka yako umeitoa kwa nia njema, nyie wote wawili – mtoaji na mpokeaji, mnapata furaha kubwa moyoni. Furaha hii hupelekea miili yenu kufurika homoni za raha (oxytocin, serotonin, na endorfins). Faida zinazoletwa na homoni hizi kiafya tumezitaja tayari hapo juu.

Kwa kumalizia kipengele hiki ni muhimu kila mmoja wetu akajua kuwa anapokuwa na mgonjwa atakuwa amemsaidia sana mgonjwa huyo kupona haraka iwapo atajitahidi kumfariji kwa sadaka. Sadaka iliyo bora kwa haja hii ni ile inayomuonyesha mgonjwa kuwa anapendwa na kuthaminiwa. Anza kwa kumsabahi mgonjwa kwa tabasamu, kisha mguse, mwombee duah, na baada ya duah muulize hali na kuanza kumsikiliza kwa umakini. Mfululuzo wa vitendo hivi utamfanya mgonjwa kuzalisha mafuriko ya homoni tulizozitaja hapo juu mwilini mwake na matokeo yake kasi ya mwili kujikarabati itaongezeka.



No comments:

Post a Comment