Wednesday, June 8, 2016
NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA: CONNECTION YA USAFI
NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA
Daktari yeyote atakuambia umuhimu wa usafi katika kutunza afya. Daktari wa meno atakuelezea umuhimu wa kusafisha kinywa mara kwa mara, tena kwa dawa. Daktari wa macho atakuelezea umuhimu wa kunawa uso kwa sabuni mara kwa mara. Daktari yeyote awaye atakuelezea umuhimu wa kunawa mikono kabla ya kula, na umuhimu mkubwa wa kusafisha matunda na mbogamboga kwa kina, kabla ya kuzila katika hali yake ya ubichi.
Madaktari wengi wanachukulia kuwa watu wengi wanajua umuhimu wa kusafisha miili yao (kuoga), na kwa hivyo hawahangaiki sana kulizungumzia hili. Hata hivyo nafasi hiyo imechukuliwa na makampuni ya kutengeneza bidhaa za usafi kuanzia yale yanayotengeneza sabuni, hadi yale yanayotengeneza mabomba ya maliwatoni. Makampuni ya kutengeneza sabuni za kuogea zenye mchanganyiko wa kemikali za kuua vimelea yanajaribu kuwafanya watu waamini kuwa siyo tu kuwa kuoga ni muhimu, lakini kuoga huko kunakuwa na maana zaidi iwapo muogaji atatumia bidhaa zao kwa sababu atakuwa anajikinga na maradhi pia!
Watengenezaji wa nepi zisizorudiwa (disposable) na pedi za kina mama za kuwasitiri wakati wa hali zao za kila mwezi, pamoja na mambo mengine, pia wanalenga kukubalika kwa bidhaa zao kwa kigezo cha kumrahisishia mvaaji suala la usafi. Bidhaa hizo hutangazwa kuwa hunyonya maji ndani zikimwacha mvaaji akiwa mkavu na mwenye furaha! Hawajakosea. Uoto wa kuvu (fungus) na uzalianaji wa bakteria wa aina nyingi hupendelea sana mazingira ya unyevunyevu wenye uvuguvugu.
Japokuwa kwa huku Afrika suala la kufunga mifereji maalum maliwatoni (bidets) kwa ajili ya kutumia maji kujisafishia baada ya haja kubwa bado halijashika kasi na hasa kwenye maofisi mengi, lakini kwa nchi za Ulaya na nyingine zilizoendelea, jambo hili linakuja kwa kasi. Nia ni ileile. Kuhakikisha kuwa kuvu na bakteria waliotoka tumboni wakiambatana na haja kubwa wameondoshjwa katika mazingira ya mwili bila kupewa nafasi ya kuzaliana na kusambaa.
Hata hivyo madaktari wanapaswa kutoicha hii kazi ya kuhimiza usafi wa mwili kwa makampuni pekee. Sababu ya kusema hivi ni kwamba madaktari ni watu wenye hadhi kubwa kwenye jamii na ambao wanaaminika na kukubalika sana. Kwa upande mwingine watu wengi wana taswira kuwa makampuni mengi yanafanya udanganyifun katika matangazo yao, kwa nia ya kuuza bidhaa tu.
Kwa mfano, hakuna kampuni hata moja itakayohangaika kukueleza kuwa moja ya faida kubwa sana za kuoga maji ni kuondoa umeme wa chembechembe chanya (positive charge) ambao unajikusanya kwenye ngozi kutokana na mwili kusuguana na hewa kila viuongo vya mwili vinapofanya mwondoko, na wakati tunapovaa nguo, hasa zile ambazo siyo za pamba kwa asilimia mia moja.
Maelezo haya hayana faida yoyote kiuchumi, hivyo tusitarajie kampuni yoyote ikapoteza muda wake kutufikishia. Hata hivyo kwa kuwa madaktari ni walinzi wa afya zetu, kwa kutufikishia ujumbe huu ni suala la wajibu.
Ukweli ni kwamba wale wanaofanya ibada na kulazimika kunawa maji mara kwa mara kwa sababu hiyo kwa kweli wanafaidika sana kiafya kwa tendo hili. Lakini kufaidi kwao hakuishii hapo. Kwa kuwa hawawezi kuosha miguu wakiwa na viatu miguuni, hulazimika kuvua viatu hivyo wakati wa kujisafisha. Tafiti za hivi karibuni zinaonyesha kuwa moja ya mambo yenye manufaa sana kiafya ni kutafuta muda walau wa nusu saa hivi kwa siku, na kutembea peku peku! Moja ya matukio ya kila wakati ndani ya miili yetu ni mlundikano wa chembechembe za umeme chanya (positively charged free radicals) ambazo kiafya zina madhara makubwa sana. Chembechembe hizi zinasababishwa na harakati nyingi zinazotokea mwilini hususan zile zinazohusiana na kuchakatua chakula.
Tafiti zimebaini kuwa kutembea pekupeku katika namna ambayo nyayo zitaunganika na udongo (haijalishi kuwa vitu hivi vinaweza kuwa vimetenganishwa na zege, saruji na hata marumaru), kutatengeneza mkondo wa umeme wa chembechembe hasi (electrons) kumiminika kuelekea mwilini, kwa ajili ya kupooza chembechembe chanya (neutralize) ndani ya mwili! Kabla ya ugunduzi huu watu walikuwa wanahimizwa kula vyakula vilivyosheheni vizuia vioksidishaji (anti oxidants), kama njia pekee ya kujilinda dhidi ya mlundikano wa chembe chanya mwilini.
Kuna suala la tohara kwa wanaume. Leo kuna kampeni kubwa ya kuzishawishi jamii mbalimbali ambazo kwa utamaduni wao hawana mila na desturi ya kutahiri, washiriki kitendo hiki. Kisa? Tafiti mbalimbali zimeonyesha kuwa maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa watu waliotahiri ni kidogo ukilinganisha na wale ambao hawajatahiriwa! Kwa maneno mengine, kutahiriwa sasa kunachukuliwa kama mkakati maalum wa kupunguza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwenye jamii. Hadi miongo michache iliyopita suala hili lilikuwa likichukuliwa kama ni la kiimani zaidi.
Japokuwa usafi ni suala la jumla, lakini kwa baadhi ya watu, kwa mfano Waislamu, ni suala la kiibada pia. Kuthibitisha hili kuna msemo unaosema ‘Uislamu ni usafi’. Waislamu wanaofanya ibada wanalazimika kufanya usafi wa vioungo vyao vya mwili kwa maji kila wakati, na hujichunga sana wasibaki na mabaki ya haja ndogo au kubwa katika maungo yao. Aidha suala la kutahiri kwao siyo kampeni ya kupunguza maambukizi ya ukimwi bali ni agizo la Mwenyezimungu kwao pale alipowaambia washikamane na mila ya Ibrahimu.
Waislamu wanaofanya ibada wamekuwa wakinufaika sana kiafya na ibada hii ya ‘usafi’, na kwa kweli wanadhulumu nafsi zao kama hawataki kufikisha faida hizi kwa wanaadamu wenzao, ambao ama ni waislamu wenzao ambao bado hawajajaliwa kushikamana na ibada, ama ni watu wa imani zingine, ambao kama walivyo wao, nao pia ni wakaazi wa dunia hii.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)






No comments:
Post a Comment