Wednesday, June 8, 2016

SIRI YA BOGA





Boga ni chakula madhubuti ambacho kimejaa viini lishe muhimu kama vile vitamini, madini lishe, na vizuia vioksidishaji. Kutokana na mchanganyiko huu wa kipekee wa virutubisho, boga lina uwezo wa kushusha shinikizo la damu (blood pressure) na kuboresha siha ya mfumo wa moyo na mishipa ya damu.

Utafiti uliofanyika hivi karibuni juu ya faida za boga kiafya ulibaini kuwa boga lina uwezo mkubwa wa kudhibiti ongezeko la sukari kwenye damu. Watafiti waliohusika waligundua kuwa boga linasaidia sana kudhibiti ongezeko la sukari kwenye damu kwa kuchochea ukarabati wa seli za kuzalisha homoni ya insulin. Seli hizi zinazojulikana kitaalamu kama ‘beta’ kuna wakati zinafanya kazi chini ya kiwango kutokana na kuharibika au kuchoka sana (fatigue).

Matokeo ya utafiti huu ambayo yamechapishwa katika jarida la kitaalamu la ‘Journal of the Science of Food and Agriculture’ yanatoa hitimisho kuwa kuchanganya boga kwenye mlo kunaweza kuwasaidia wagonjwa wa kisukari cha ukubwani (Type II Diabetes) kudhibiti ugonjwa huo hatari.

Faida nyingine kubwa ya kiafya ya boga ni uwezo wake wa kushusha kiwango cha lehemu (cholesterol) kwenye damu na kuratibu kiasi cha mafuta aina ya ‘triglyceride’. Baadhi ya aina za mafuta haya hutuhumiwa kuwa na athari mbaya katika mfumo wa moyo na mishipa ya damu.

Aidha imebainika pia kuwa watu wanaokula maboga mara kwa mara hawaathiriwi sana na magonjwa ya msongo (Depression) na kukosa usingizi (Imsomnia). Baadhi ya kemikali za asili zilizoko kwenye boga husaidia kuboresha hali ya usononi (mood) na kupunguza viwango vya msongo (stress).

Pamoja na nyama ya boga kuwa na manufaa makubwa kiafya, mbegu za boga ni zenye manufaa zaidi.

  1. Mbegu za boga ni chanzo kizuri sana cha madini lishe kama vile zinc, phosphorous, magnesium na manganese.
  2. Mbegu hizo pia zina wingi wa vitamini E.
  3. Mbegu hizo pia zina mchanganyiko mwanana wa virutubisho vinavyimarisha afya ya mfumo wa moyo na mishipa ya damu ikiwa ni pamoja na wingi wa vizuia vioksidishaji na tindikali ya phenol (Phenolic acid)
  4. Mbegu hizi pia ni bora sana katika kulinda afya ya tezi kibofu (prostate gland)
  5. Mbegu za boga pia ni chanzo kizuri sana cha nyuzi lishe (dietary fibre) mafuta koza kiasi (mono-saturated fatty acids), ambavyo kwa pamoja hufanya kazi nzuri kuboresha afya ya moyo na ubongo.

Kiasi cha gramu 100 za mbegu za boga kitakupa viwango vifuatavyo vya virutubisho:

  1. Calori 559 za nishati;
  2. Gramu 30 za protini;
  3. 110% ya mahitaji ya siku nzima ya madini lishe ya chuma;
  4. 71% ya mahitaji ya siku nzima ya madini lishe ya zink;
  5. 17% ya mahitaji ya siku nzima ya madini lishe ya selenium;

Aidha kiasi hiki pia kitakupatia kiasi cha kutosha cha kijenzi muhimu sana cha protini (Amino acid) kinachoitwa tryptophan. Tryptophan ndiyo kiambata (ingredient) muhimu katika uzalishaji wa homoni ya serotinin. Serotini ni homoni muhimu ambayo inachochea hali ya utulivu, kujisikia raha na usingizi. Kwa kawaida mwili hauna uwezo wa kuzalisha tryptophan yake wenyewe hivyo tunaipata tu kupitia baadhi ya vyakula kama hizo mbegu za boga.


1 comment: