Wednesday, June 8, 2016

NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA: CONNECTION YA FAMILIA


NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA

Wakati nikiwa mwanafunzi siku moja nilikuwa naongea na Profesa mmoja kutoka Sweden akaniambia kuwa sisi Waafrika tuna bahati sana lakini hatujitambui. Nilipoomuliza ni kwa nini anasema hivyo akaniambia kuwa bahati tuliyokuwa nayo ni ile ya kuwa ‘pamoja’ katika mambo yetu mengi, kitu ambacho huko kwao uzunguni kwa kiasi kikubwa kilikuwa kimetoweka.

‘Nilipofika hapa kwa mara ya kwanza nilishangaa sana. Mnakutana barabarani wawili – hamkuwa na appointment wala nini – lakini mnapoteza dakika mbili tatu kupeana salammu na kuulizana habari! Unamuuliza mtu njia, anaona kuwa kukuelekeza tu kwa mdomo haitoshi, anaamua kuacha alichokuwa anafanya akupeleke huko unakotaka kwenda kabisa kabisa! Baada ya kukaa kwa siku chache hii hali iliniathiri na kwa mara ya kwanza katika maisha yangu nikajiona kama naishi katika jamii ya wanadamu! Ni kweli Waafrika mnahitaji kuongeza ufanisi katika shughuli zenu, lakini ufanisi wenyewe sio wa kutuiga sisi. Sisi tumeshaharibikiwa vibaya!’

Haya ni maneno aliyoyatumia Profesa Aeglifeat, kama sijasahu, nadhani hilo ndilo lililokuwa jina lake, ingawa nina hisia nzito kuwa tahajia (spelling) ya jina lake nitakuwa nimeikosea. Nilipomuuliza kuwa kwani kule kwao hali ilikuwaje hadi yeye kufikia kusema hivyo alijibu.

‘ Kabla sijaondoka kule Sweden kuja huku, serikali ilifanya utafiti kuhusu matatizo ya kiafya ya wazee ambayo yalikuwa yanaigharimu fedha nyingi sana! Ilichogundua ni kwamba wazee wengi hawakuwa na maradhi halisi, bali walikuwa wanaugua upweke! Sasa upweke unatibiwaje? Baada ya tafakuri serikali ikagundua suluhisho la tatizo hilo. Suluhisho lenyewe lilikuwa ni kuwatafuta watoto wa wazee hao popote walipo waingie makubaliano na serikali kulipwa kiasi fulani cha posho, ili katika nyakati fulani fulani wakawazuru wazee wao. Kwa hesabu za serikali mkakati huu ulikuwa na gharama nafuu zaidi kuliko gharama ya dawa ambayo serikali ilikuwa inalazimika kuingia kwa niaba ya wazee hao! Sasa kama huku siyo kuharibikiwa ni nini? Hebu fikiria, ulipwe ndiyo ukamtembelee mzazi wako?!’

Waandishi Ptak na Duncan (2001) wanaulelezea upweke kuwa ni hali inayoambatana na msongo mkali inayotokana na kuwekwa pembeni kimaono (emotionally) au kijamii (socially). Wanaendelea kuelezea kuwa kuwa mpweke au kutokuwa mpweke siyo suala la kuzungukwa na watu karibu; bali ni suala la ubora wa mahusiano baina yako na hao wanaokuzunguka.

‘Uchungu wa mwana aujua mzazi!’ ni msemo ambao ni kielelezo halisi cha hali hii. Hakuna awezaye kuchukua nafasi ya mzazi, na wala hakuna awezaye kuchukua nafasi ya mtoto wa kuzaa. Muunganiko wa kibaiolojia wa hawa watu wawili una nguvu mno. Mzazi wa mwenzako hata ungemtendea wema wa aina gani, pamoja na kukushukuru kwa dhati, bado atatamani kama wema huo angekuwa anatendewa na mwanae wa kuzaa, na vivyo hivyo kwa mtoto. Mtoto yatima, haijalishi atalelewa kwa upendo kiasi gani, pamoja na kufurahia upendo huo, ndani ya moyo wake bado atatamani sana kuwa huyo anayemlea angekuwa ni mzazi wake wa kumzaa. Na hiki ndicho kilichokuwa kinawaathiri hao wazee wetu wa Kisweden. Serikali ilikuwa inajitahidi kuwapa kila kitu, lakini haikutosha. Mioyo yao ilikuwa inatamani kuwaona watoto wao, wazungumze nao, japo kwa muda kidogo tu!

Je, upweke unaathiri vipi afya za watu? Wataalamu wanasema upweke huchochea mwili kuzalisha homoni (hormones) ambazo huathiri mifumo ya mwili katika hali ambayo ni hasi. Waandishi Ptak na Duncan (2001) wanasema miongoni mwa magonjwa yanayotokana na upweke ni vidonda vya tumbo, pumu, kiharusi, mfadhaiko, maumivu mfululuzo ya kichwa, magonjwa ya moyo, ulevi, hamu ya kujiua, na magonjwa ya mfumo wa kinga za mwili. Aidha wanasema upweke mara nyingi hutuzuia tusipone, au tusipate nafuu katika maradhi yanayotusumbua.

Kutokana na matatizo haya ya upweke uliopindukia, leo uzunguni wamebuni utaratibu wa tiba unaotumia wanyama (Animal Assisted Therapy). Baadhi ya vipengele vya utaratibu huu ni kuwatumia wanyama mbalimbali kuwa karibu na watu mbalimbali wenye matatizo ya kiafya, kitendo ambacho tafiti zimeonyesha kuwa kinasaidia sana kutoa ahueni kwa mgonjwa. Kusema ule ukweli huko uzunguni wamefikia hatua hiyo kwa kule kudhani kwao kuwa hawamuhitaji tena Mungu! Mungu amebaki kama kielelezo cha misimu ya sherehe, lakini siyo kwa kutoa miongozo ya jinsi ya kuishi katika hii dunia.

Moja ya ibada kubwa kabisa ni kuwaheshimu wazazi wawili, na kuwatumikia bila kinyongo hadi pale watakapoondoka juu uso huu wa dunia. Kwa mtizamo huu wa kidini, jukumu la kuwatunza wazazi wazee siyo la jamii bali ni la watoto wao. Kama ambavyo Wasweden wamegundua wakati washachelewa, watoto ni dawa kubwa sana kwa wazazi wao pale wanapokabiliwa na maradhi ya uzee.

Suala la kuwatendea wazazi wema na ihsani ni suala ambalo limesisitizwa sana na dini. Mathalani baadhi ya maelekezo ya Uislamu kuhusu suala hili ni haya yafuatayo:

‘Muabuni Mwenyezi Mungu na wala msimshirikishe na chochote, na wafanyieni ihsani wazazi wawili, na jamaa na mayatima na maskini’ (Quran 4:36)

‘Na mola wako amehukumu kuwa msimuabudu yeyote ila yeye tu. Na (ameagiza) kuwafanyia wema (mkubwa) wazazi. Kama mmoja wao akifikia uzee, (naye yuko) pamoja nawe, au wote wawili, basi usiwaambie hata “Ah!” wala usiwakemee. Na useme nao kwa msemo wa heshima (kabisa). Na uwainamishie bawa la unyenyekevu (njia ya kuwaonea) huruma (kwa kuwaona wamekuwa wazee). Na useme “Mola wangu! Warehemu (wazee wangu) kama walivyonilea katika utoto” (Quran 17: 23-24)

‘Wanakuuliza watoe nini? Sema: “Mali yoyote mtakayotoa (itoeni) muwape wazazi, na ndugu, mayatima, na masikini, na wasafiri (walioharibikiwa), na waliokuwa (kama hawa). Na wema wowote mnaofanya Mwenyezimungu anajua’ (Quran 2: 215)

‘Na tumemuusia mwanaadamu afanye wema kwa wazazi wake. Mama yake amechukua mimba yake kwa taabu na akamzaa kwa taabu. Na amebeba mimba yake hadi kumwachisha ziwa ; (uchache wake) ni miezi thelathini. Na hata anapofikia balekhe yake na akawa mwenye umri wa miaka arobaini (mtoto mwema) husema : “Ewe Mola wangu! Niwezeshe nishukuru neema zako ulizonineemesha mimi na wazazi wangu, na niwezeshe nifanye vitendo vizuri unavyovipenda, na unitengenezee watoto wangu; kwa yakini ninatubu kwako; na hakika mimi ni miongoni mwa waliosilimu (walionyenyekea).” (Quran 46:15)

Kwa kuzingatia maelekezo haya ya Quran tukufu, na bila shaka kwa kuungwa mkono na maelekezo ya vitabu vya dini nyingine ambazo chimbuko lake ni Mungu mmoja, suala la watoto kuwafanyia wazazi wao wema na ukarimu ni miongoni mwa ibada kubwa kabisa. Kila mwenye kutekeleza ibada hii ajue kuwa amempa pia mzazi wake au wazazi wake, dawa kubwa na ya kipekee; ambayo bila ya shaka yoyote itaboresha sana ubora wa maisha kiafya kwa wazazi wake.


No comments:

Post a Comment