Wednesday, June 8, 2016

NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA: CONNECTION YA LISHE (HALALI, NZURI NA KIASI)



NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA

Tunapozungumzia lishe suala la uhalali au uharamu halipimiki kwa kipimo sawa kwa kila mtu. Ni suala linalotegemea zaidi utamaduni wa jamii mbalimbali tofauti, na au imani za dini. Uhalali au uharamu katika lishe unaoegemea kwenye utamaduni fulani, ni tofauti na ule uhalali au uharamu unaoegemea kwenye imani ya dini. Uhalali au uharamu katika lishe unaoegemea kwenye utamaduni hubadilika kulingana na mabadiliko ya utamaduni husika, tofauti na ule unaoegemea kwenye imani za dini ambao unakuwa ni wa kudumu, ukiwa ni sehemu muhimu ya mafundisho ya dini husika.

Kwa mfano, Wamaasai wa zamani walikuwa hawali samaki wala kuku. Sehemu kubwa ya utamaduni wa Kimaasai miaka hiyo ulijifunga kwenye ufugaji wa ng’ombe. Chakula halali kwa Wamaasai wa enzi hizo kilikuwa ni kile kinachotokana na wanyama hao – nyama, maziwa, damu na samli. Leo hii utamaduni uliojifungamanisha na ufugaji wa ng’ombe kwa kiasi kikubwa umesambaratika. Leo vijana wengi wa kimaasai wanakimbilia mijini kufanya kazi za ulinzi, ususi wa rasta za kimaasai, na uuzaji wa miti shamba. Kutokana na vijana hawa kutokuwa tena na mahusiano ya karibu na ng’ombe, leo wanakula kuku, samaki, na hata nafaka mbalimbali.

Kwa upande wa pili, pamoja na mabadiliko yote yanayotokea katika jamii – kiutamaduni, kielimu, kitekinolojia, nakadhalika – Wakristo wa madhehebu ya Kisabato hadi leo lishe yao inaamuliwa na maandiko katika vitabu vyao vya dini. Ukimkuta Msabato kwa mfano anakula samaki wasio na magamba, basi ujue kuwa huyo ni mwasi tu, na wala ulaji wake huo hauwakilishi mabadiliko yoyote ya kilishe katika dhehebu hilo kwa ujumla. Vivo hivyo kwa waumini wa dini ya Kiislamu. Mafundisho ya dini ya kiislamu yanatakaza ulaji wa vyakula kadhaa, kwa mfano nyama ya nguruwe. Sasa pamoja na kwamba tuko kwenye karne ya ishirini na moja, karne ya sayansi na tekinolojia, tena katika kipindi ambacho upashanaji wa habari kwa kasi (information age) ndio njia kuu ya uchumi, hutamkuta Muislamu akila nguruwe hadharani kwa sababu limetoka tamko la jumla kutoka kwa wanazuoni wa dini hiyo kwamba sasa ‘kiti moto’ ni halali. Ukimkuta Muislamu huyo basi ni mwasi tu, kama ambavyo yule Msabato alaye samaki asiye na magamba alivyo mwasi kwa dhehebu lake.

Kwa kuwa suala la afya njema ni suala linalotegemea, pamoja na mambo mengine, lishe bora na wala siyo utamaduni wala dini ya mtu, hebu suala la uhalali tulijadili, tukiwa tumelifungamanisha na suala la uzuri (ubora). Kwa muktadha huu, chakula kinaweza kikawa ni halali lakini kikawa siyo kizuri (bora). Kwa mfano maziwa ni chakula ambacho ni halali kabisa kwa itikadi ya dini zote, hata Mabaniani. Hata hivyo ubora wa maziwa unategemea kama yamesindikwa ama la. Maziwa yaliyosindikwa kwa nia ya kuyapa uhai wa muda mrefu madukani (long shelf life) siyo chakula bora. Sababu ya kukosa ubora ni kuwa katika usindakaji huo maumbile la baadhi ya virutubisho kwenye maziwa hayo hubadilika, na mabadiliko hayo yanawadhuru baadhi ya walaji bila wenyewe kujitambua. Madhara haya mara nyingi yanakuja katika mtindo wa mzio (allerge), na mtumiaji anaweza akahangaika sana kabla ya kugundua kuwa kinachomsumbua ni utumiaji wa maziwa yaliyosindikwa!
Mfano mwingine ni nyama, mathalani ya ng’ombe. Nyama husika inaweza kuwa imepatikana baada ya ng’ombe kuchinjwa kwa taratibu zote za Kiislamu, na kwa maana hiyo ikawa ni halali kuliwa na kila mtu. Sasa mtu akichukua nyama hiyo akaenda kuchoma mishikaki, bila kuchukua tahadhari stahiki, uhalali wa nyama hiyo utabaki pale pale, lakini mishikaki husika haiwezi kuitwa ni chakula kizuri. Hii ni kutokana na ukweli kuwa uchomaji wa mishikaki ni aina ya upishi ambao unahitaji tahadhari nyama isije ikaungua na kufanya mkaa. Maeneo yaliyofanya mkaa ni maeneo ambayo yametengeneza sumu mbaya zinazodhuru afya. Sumu hizi zinaitwa ‘Hetero cyclic Amines’. Sumu hizi zinatajwa kuwa ni miongoni mwa vichocheo vikubwa vya ugonjwa wa saratani. Wataalamu wanaeleza kuwa kuipaka nyama husika vioungo kama manjano (turmeric) na majani ya rosemary husaidia kupunguza athari hizo.

Mfano mwingine ni unga wa sembe. Unga wa sembe ni halali, na tena unapendeza machoni. Hata hivyo unga huo ni chakula kisicho na ubora wowote; sana sana ni chakula chenye muelekeo mkubwa wa kukuletea maradhi. Ni chakula ambacho nyuzi-lishe pamoja na viini lishe vingine vimeondolewa na kubakiwa na wanga mtupu. Wanga huu mtupu unapoingia mwilini bila kuambatana na viini lishe vilivyoondolewa husababisha kinga za mwili kuhisi kuwa mwili umevamiwa; na kuanza kujipanga kutoa ulinzi. Kitendo hiki husababisha seli zote za mwili kuvamiwa na uvimbe mwako (inflammation), hali ambayo iwapo itadumu kwa muda mrefu, ina madhara makubwa sana kiafya mwilini.

Mifano ni mingi mno ya vyakula halali lakini visivyo na ubora. Watu wanachotakiwa kuzingatia ni kwamba dhana hizi mbili ni lazima ziende pamoja. Dhana ya tatu inayoambatana na dhana hizi pacha, ni kanuni ya ‘kiasi’. Chakula kinaweza kikawa ni halali na chenye ubora unaotakiwa, lakini kikawa na madhara makubwa kwa mtumiaji kutokana na kutokuzingatia kanuni hii ya ‘kiasi’ wakati wa kukila. Kanuni ya kiasi inatuhitaji kula kiasi cha chakula na kuacha sehemu nyingine ya tumbo ikiwa wazi kwa ajili ya maji na hewa. Ukweli wa kanuni hii unadhihiri pale unapomkuta mtu amekula vyakula vingi na vya aina tofauti tofauti kwa wakati mmoja, hadi akashiba sana. Kinachofuata hapa ni kuvimbiwa. Unafuu utapatikana tu pale ambapo mhusika atatapika. Kitendo cha kutapika ni ujumbe unaoletwa na tumbo kwamba ‘ Umenijaza sana nashindwa kufanya kazi!’

Kula kiasi kuna umuhimu mkubwa sana kiafya. Hii ni kutokana na ukweli kuwa seli zako za mwili zinahitaji kiasi fualani tu cha virutubisho ili ziweze kufanya kazi zake kwa ufanisi. Ziada yoyote au itageuzwa kuwa mafuta yahifadhiwe mwilini (kama hiyo ziada inatoka kwenye wanga), au itageuka kuwa sumu mbaya mwilini na kukusababishia madhara mengi, kama hiyo ziada inatoka kwenye protini. Mafuta yanapohifadhiwa mwilini kwa wingi huzaa unene uliopindukia, na unene uliopindukia huzaa magonjwa mengi ya kimfumo; ikiwa ni pamoja na shinikizo la damu, kisukari cha ukubwani, ugonjwa wa moyo, nakadhalika. Kwa upande wa pili, mwili unapokuwa umezidiwa na sumu zinazotokana na mabaki ya protini hupelekea mwili huo kujaa tindikali; tindikali ambayo hujenga mazingira bora ya kustawisha kuzaliana kwa wingi kwa vijidudu vinavyoambukiza maradhi, na pia kuzichochea seli za mwili kujibadili na kuwa seli za saratani!

Kula vyakula halali, vizuri, na kwa kiasi ndiyo pia maagizo ya Mungu Muumba. Na huu ndio msingi wa kusema ibada inalinda siha, kwani ibada ni kufuata maagizo ya Mwenyezi Mungu. Katika Uislamu kuna mafundisho yafuatayo yanayohusiana na lishe kulingana na maelezo tuliyoyatanguliza:

“Enyi mlioamini! Kuleni vizuri na halali tulivyokuruzukuni, na Mumshukuru Mwenyezi Mungu, ikiwa ni kweli mnamuabudu” (Quran 2:172)

“Enyi watu! Kuleni vilivyomo katika ardhi, halali na vizuri, wala msifuate nyayo za shetani. Bila ya shaka yeye kwenu ni adui aliye dhahiri” (Quran 2: 168)

“Yeye amekuharamishieni mzoga tu, na damu, na nyama ya nguruwe, na nyama ya mnyama ambaye wakati wa kuchinjwa kwake hakutajiwa jina la Mwenyezi Mungu pekee. Lakini aliyefikwa na dharura (ya kula vitu hivi) bila kutamani wala kupita kiasi, yeye hana dhambi. Hakika Mwenyezi Mungu ni mwingi wa kusamehe (na) mwingi wa kurehemu.” (Quran 2:173)

“ Enyi wanaadamu! Chukueni mapambo yenu wakati wa kila sala; na kuleni (vizuri) na kunyweni (vizuri). Lakini msipite kiasi tu. Hakika yeye (Mwenyezi Mungu ) hawapendi wapitao kiasi.” (Quran 7:31)

Katika kusisitiza umuhimu wa kula kiasi tu, Mtume Muhammad (SAW) amesema:
“Udhaifu mkubwa wa mwanadamu ni katika tumbo lake. Kama ni lazima ule basi gawanya tumbo lako katika sehemu tatu. Tumia sehemu moja kwa chakula, na bakiza sehemu mbili zilizobaki kwa ajili ya maji na hewa”

Na katika hadithi nyingine, bwana Mtume (SAW) amenukuliwa akisema:
“ Tumbo ni tangi la mwili na mishipa mbalimbali ya damu huelekea huko. Tumbo linapokuwa na siha mishipa ya damu hutoka huko ikiwa na afya njema, lakini tumbo linapokuwa na maradhi mishipa hiyo hutoka huko ikiwa imebeba magonjwa”


No comments:

Post a Comment