Wednesday, June 8, 2016
NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA: CONNECTION YA TOHARA (JANDO)
NGUVU YA IBADA KATIKA KULINDA SIHA NJEMA
Kwa mujibu wa Shirika la Afya duniani, tohara (kutahiri) inatakiwa kuwa ni sehemu muhimu katika vita ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi. Watafiti wa masuala ya afya wanadai kuwa kitendo cha kutahiri kinampunguzia mwanamme uwezekano wa kuambukizwa virusi vya ukimwi anapokutana kingono na mwanamke aliyeathirika kwa kiasi cha asilimi sitini (60%)!
Katika kitabu chake, ‘al –Khitaan’, Dk. Muhammad Ali al Baar, ambaye ni mwanachama wa Chuo cha Kifalme cha Madaktari Bingwa wa Upasuaji cha Uingereza, na mshauri kwenye idara ya Tiba za Kiislamu katika Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Mfalme Fahdi katika Chuo Kikuu cha Mfalme Abdul Aziz, kule Jeddah Saudi Arabia, ametaja faida za ziada za tohara inayofanywa kwa watoto wakiwa wangali wadogo kama ifuatavyo:
1. Ni kinga dhidi ya maambukizi ya kwenye uume (dhakar) sehemu ya nje;
2. Ni kinga dhidi ya maambukizi ya kwenye uume sehemu ya ndani (kwenye njia ya mkojo). Tafiti zimeonyesha kuwa asilimia tisini na tano (95%) ya watoto wanaopata maambukizi katika njia ya mkojo ni wale ambao hawakutahiriwa.
3. Ni kinga dhidi ya saratani ya kwenye uume. Tafiti mbalimbali zimebainisha kuwa saratani ya kwenye uume ni kama haipo kabisa miongoni mwa wanaume ambao wametahiriwa. Katika nchi mbazo viwango vya kutahiriwa viko chini kama China, Uganda, na Puerto Rico, saratani za kwenye uume ni kati ya 12-22% ya saratani zote zinazowakumba wanaume!
4. Ni kinga dhidi ya magonjwa mengi ya zinaa. Watafiti wamebaini kwamba magonjwa ya zinaa kama vile gonoria, kaswende, muasho, nakadhalika, husambaa kwa kiwango kikubwa zaidi kwa wanaume wasio tahiriwa ikilinganishwa na wale waliotahiriwa.
5. Ni kinga dhidi ya saratani ya kizazi kwa wanawake. Tafiti zimebaini kuwa wake wa wanaume waliotahiriwa wako katika hatari ndogo zaidi ya kupata saratani ya kizazi, ikilinganishwa na wake wa wanaume ambao hawajatahiriwa.
Kwa kuwa huyo aliyrtuumba yote haya anayajua, bila ya shaka ndio maana akafanya kutahiriwa kuwa ni miongoni mwa ibada kubwa kabisa. Mwenyezi Mungu muumba katika Quran 16:123 anatuambia:
‘Kisha tukakufunulia kuwa ufuate mila ya Ibrahim (aliyekuwa) mtii kamili, wala hakuwa miongoni mwa washirikina’
Inajulikana kuwa sehemu muhimu ya mila ya Ibrahim ilikuwa ni kutahiriwa. Mtume Muhammad (SAW) katika hadithi iliyotajwa na Bukhari, Muslim na Ahmad amesema:
‘Nabii Ibrahim (amani iwe juu yake) alijitahiri yeye mwenyewe akiwa na umri wa miaka themanini na alifanya hivyo kwa kutumia shoka’
Aidha mtume Muhammad (SAW) kuhusu tohara ameendelea kusema:
‘Kuna mambo matano ambayo ni ya asili kwa mwanaadamu: Kutahiriwa, kunyoa nywele za kinenani, kukata kucha, kuonyoa nywele za makwapani, na kunyoa sharubu.’
Ukweli wa kauli hii ya mtume (SAW) unadhirishwa na uchunguzi wa tabia za baadhi ya makabila ya asli ya bara la Afrika, kwa mfano Wamaasai na Wakurya. Kitendo cha kuingia jando (kutahiri) kwa makabila hayo ni mila yenye nguvu mno ambayo chimbuko lake halijulikani. Kinachojulikana ni kwamba mila hii ilikuwepo kwa makabila haya kabla kabisa ya kufikiwa na Uislamu; hivyo makabila haya hayawezi kuambiwa kuwa yamejifunza mila hii kutoka kwenye Uislamu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)






No comments:
Post a Comment