Monday, February 27, 2017

JE, TUNAJIAMBUKIZA SARATANI KILA KUKICHA?!



Kitaalam inaaminika kuwa saratani ni ugonjwa wowote unaojitokeza baada ya seli za kawaida za mwili kuharibika na kushindwa kufa kwa ‘kasi’ inayotakiwa katika utaratibu maalum unaoitwa apoptosis. Apoptosis ni kifo cha seli kilichopangwa katika utaratibu maalum, au kwa kiingereza, programmed cell death.

Seli hizi zilizopoteza mwelekeo na kugoma kufa, huendelea na mchakato wa   kugawanyika kama zinavyofanya seli nzima ambazo hazijaharibika. Hata hivyo kutokana na kuwa mbovu, seli hizi hizi hugawanyika kiholela na kwa kasi kubwa; hali ambayo hupelekea kuundwa kwa tishu za saratani.
Ni kwa nini seli za kawaida za mwili huharibika?

Mambo kadhaa yanaweza kusababisha seli za mwili kuharibika. Miongoni mwa mambo haya ni pamoja na:

1.      Kukosa kiasi cha kutosha cha gesi ya oxygen.
Sehemu kubwa ya seli za mwili zina asili ya kutumia gesi ya oxygen katika mchakato wa kuzalisha nishati kwa ajili ya seli kujiendesha. Mazingira ya seli yenye ufinyu wa gesi ya oxygen yanaweza kusababisha seli kubadili muundo wake ili iweze kuendelea kuishi bila kuhitaji gesi hiyo ya oxygen. Kwa bahati mbaya mabadiliko haya huzaa seli za sataratani.

2.      Msongo endelevu
Tafiti zimebainisha kuwa homoni zinazozalishwa na mwili ili kukabiliana na msongo, hasa pale msongo wenyewe unapokuwa endelevu, huchangia katika uharibifu wa sehemu ya seli inayobeba vinasaba (DNA). Wataalamu wanasema iwapo uharibifu husika utakuwa umegusa sehemu ya kinasaba ya kuamrisha seli kujiua inapokuwa imeharibika seli husika haitakufa na badala yake itageuka kuwa seli ya saratani.

Njia nyingine ambayo homoni za msongo hupelekea kustawi na kushamiri kwa kansa ni kwa kudhoofisha mfumo wa kinga za mwili. Kinadharia kinga za mwili zinatakiwa zifanye mashambulizi na kuharibu seli zote za saratani zinazoonekana mwilini. Hata hivyo imebainika kuwa katika hali halisi mfumo wa kinga za mwili haufanyi chochote kupambana na seli za saratani. Tafiti zinaonyesha kuwa homoni za msongo huamsha kinasaba kinachoitwa ATF3 ambacho huvuruga mfumo wa kinga za mwili na kuufanya ushindwe kufanya kazi yake kwa ufanisi.

3.      Carcinogens
Tafiti pia zimebainisha kuwa seli za mwili huharibika pia pale vitu fulani fulani vinavyojulikana kitaalamu kama carcinogens vinapoharibu vinasaba katika seli husika, au kuvuruga michakato mbalimbali ya uvunjifu na ujenzi wa kemikali ndani ya seli hizo (cellular metabolism). Kama ilivyo kwa uharibifu unaofanywa na homoni za msongo, iwapo uharibifu husika utakuwa umegusa sehemu ya kinasaba yenye kuelekeza seli kujiua iwapo imekumbwa na uharibifu, seli hiyo itashindwa kujiangamiza na hivyo kugeuka kuwa seli ya saratani.

Carcinogens zinaweza kuwa katika mfumo wa kemikali mbalimbali (ikiwa ni pamoja na zile za asili), vimelea kama bakteria, kuvu (fangasi) na virusi,  na au mionzi mbalimbali. Mifano iliyozoeleka sana ya carcinogens za kikemikali ni pamoja na:

§  Vumbi la asbestos;
§  Vumbi la fiberglass;
§  Moshi wa tumbaku;
§  Acryl-amides ambazo ni kemikali zinazopatikana kwenye vyakula vya wanga vilivyopikwa katika joto la juu sana kama chips za viazi, mikate na maandazi;
§  Heterocyclic amines ambazo ni kemikali zinazojiunda pale vyakula vya protini kama nyama vinapoungulia na kutengeneza hali ya kuwa kama mkaa;
§  Vinyl Chloride ambayo hutumika katika uzalishaji wa PVC;
§  Formaldehyde ambayo hutumiwa katika kutunzia maiti;
§  Benzene ambayo ni moja ya malighafi kubwa zinazotumiwa viwandani kwa ajili ya uzalishaji wa kemikali zinazohitajika kwa matumizi mengine mbalimbali;
§  Madini kama zebaki (mercury) na nickel; na
§  Kemikali za aina ya dioxins ambazo ni zao la ziada aghalabu pale uchomaji wa taka za majumbani na viwandani unapokuwa haukukamilika. Kemikali hizi pia huzalishwa kwa kiwango kidogo katika mchakato wa utengenezaji wa karatasi (kuzifanya ziwe nyeupe) na katika uzalishaji wa aina fulani ya kemikali zenye kiambata cha kiasili cha chlorine kama vile Polychlorinated Biphenyls (PCBs), chlorinated phenols, chlorinated benzene na baadhi ya madawa ya kuulia wadudu na wanyama waharibifu. Aidha, moshi unaotoka kwenye vipumulio vya vyombo vya usafiri (exhaust pipes), misitu inayoungua, na kuni pia huziachia kwenda hewani.
Kwa upande wa vimelea, mifano iliyozoeleka ni kama vile:
§  Aflatoxin B1, ambayo ni zao la fangasi inayoitwa Aspergillus flavus inayoota katika nafaka zilizohifadhiwa, njugu na siagi ya karanga (peanut butter);
§  Baadhi ya virusi, kama vile hepatitis B na hepatitis C vinavyohusishwa na saratani ya ini; human papilloma virus (HPV) kinachohusishwa na saratani ya shingo ya kizazi; herpesvirus 8 kinachohushwa na saratani ya ngozi; na Epstein-Barr virus kinachohusishwa na saratani aina ya lymphoma ambayo huikumba sehemu ya mfumo wa kinga za mwili inayoitwa mfumo wa lymph. 
§  Baadhi ya bakteria kama vile Helicobacter pylori ambayo inahusishwa na saratani ya tumbo pamoja na vidonda vya tumbo.
Hata hivyo ni vizuri ikaeleweka kuwa carcinogens siyo lazima zikaleta madhara kwenye seli hapohapo zinapoingia mwilini. Kuna wakati baadhi ya carcinogens hupitia njia za mzunguko kupitia mchakato au michakato kadhaa kabla ya kufanya uharibifu unaozungumziwa.

Ziko carcinogens kadhaa zinazoweza kuitwa kuwa ni za kiasili. Miongoni mwa hizi ni Aflatoxin B1, kirusi cha hepatitis B, na HPV. 

Sukari! Tafiti zimeibaini kuwa ni kianzishaji na kiendelezaji kikubwa cha saratani.

Katika utafiti uliopewa jina Increased sugar uptake promotes oncogenesis via EPAC/RAP1 and O-GlcNAc pathways na kuchapishwa tarehe 09/12/2013 katika jarida la kitaaluma la Journal of Clinical Investigation, watafiti wameonyesha kuwa sukari siyo tu kwamba ni kichocheo kikubwa cha kuongezeka na kukua kwa seli za saratani mwilini, lakini pia ni kianzilishi cha saratani katika seli ambazo hapo awali zilikuwa na siha njema.
Ni vizuri hapa ikaeleweka kuwa inapozungumzwa sukari, kinachozungumziwa ni chakula chochote ambacho kikiliwa na kuchakatwa ndani ya mwili, kina uwezo wa kusababisha ongezeko la sukari kwenye damu na hivyo kuchochea ongezeko la hormoni ya insulin ndani ya damu. Hii ina maana kuwa vyakula husika ni sukari yenyewe ya mezani na vyakula vingine vyenye uwezo huo, hususan vile ambavyo vina kiasi kikubwa cha wanga.

No comments:

Post a Comment