Monday, February 27, 2017

JE, TUNAJIAMBUKIZA SARATANI KILA KUKICHA?!



Kitaalam inaaminika kuwa saratani ni ugonjwa wowote unaojitokeza baada ya seli za kawaida za mwili kuharibika na kushindwa kufa kwa ‘kasi’ inayotakiwa katika utaratibu maalum unaoitwa apoptosis. Apoptosis ni kifo cha seli kilichopangwa katika utaratibu maalum, au kwa kiingereza, programmed cell death.

Seli hizi zilizopoteza mwelekeo na kugoma kufa, huendelea na mchakato wa   kugawanyika kama zinavyofanya seli nzima ambazo hazijaharibika. Hata hivyo kutokana na kuwa mbovu, seli hizi hizi hugawanyika kiholela na kwa kasi kubwa; hali ambayo hupelekea kuundwa kwa tishu za saratani.
Ni kwa nini seli za kawaida za mwili huharibika?

Mambo kadhaa yanaweza kusababisha seli za mwili kuharibika. Miongoni mwa mambo haya ni pamoja na:

1.      Kukosa kiasi cha kutosha cha gesi ya oxygen.
Sehemu kubwa ya seli za mwili zina asili ya kutumia gesi ya oxygen katika mchakato wa kuzalisha nishati kwa ajili ya seli kujiendesha. Mazingira ya seli yenye ufinyu wa gesi ya oxygen yanaweza kusababisha seli kubadili muundo wake ili iweze kuendelea kuishi bila kuhitaji gesi hiyo ya oxygen. Kwa bahati mbaya mabadiliko haya huzaa seli za sataratani.

2.      Msongo endelevu
Tafiti zimebainisha kuwa homoni zinazozalishwa na mwili ili kukabiliana na msongo, hasa pale msongo wenyewe unapokuwa endelevu, huchangia katika uharibifu wa sehemu ya seli inayobeba vinasaba (DNA). Wataalamu wanasema iwapo uharibifu husika utakuwa umegusa sehemu ya kinasaba ya kuamrisha seli kujiua inapokuwa imeharibika seli husika haitakufa na badala yake itageuka kuwa seli ya saratani.

Njia nyingine ambayo homoni za msongo hupelekea kustawi na kushamiri kwa kansa ni kwa kudhoofisha mfumo wa kinga za mwili. Kinadharia kinga za mwili zinatakiwa zifanye mashambulizi na kuharibu seli zote za saratani zinazoonekana mwilini. Hata hivyo imebainika kuwa katika hali halisi mfumo wa kinga za mwili haufanyi chochote kupambana na seli za saratani. Tafiti zinaonyesha kuwa homoni za msongo huamsha kinasaba kinachoitwa ATF3 ambacho huvuruga mfumo wa kinga za mwili na kuufanya ushindwe kufanya kazi yake kwa ufanisi.

3.      Carcinogens
Tafiti pia zimebainisha kuwa seli za mwili huharibika pia pale vitu fulani fulani vinavyojulikana kitaalamu kama carcinogens vinapoharibu vinasaba katika seli husika, au kuvuruga michakato mbalimbali ya uvunjifu na ujenzi wa kemikali ndani ya seli hizo (cellular metabolism). Kama ilivyo kwa uharibifu unaofanywa na homoni za msongo, iwapo uharibifu husika utakuwa umegusa sehemu ya kinasaba yenye kuelekeza seli kujiua iwapo imekumbwa na uharibifu, seli hiyo itashindwa kujiangamiza na hivyo kugeuka kuwa seli ya saratani.

Carcinogens zinaweza kuwa katika mfumo wa kemikali mbalimbali (ikiwa ni pamoja na zile za asili), vimelea kama bakteria, kuvu (fangasi) na virusi,  na au mionzi mbalimbali. Mifano iliyozoeleka sana ya carcinogens za kikemikali ni pamoja na:

§  Vumbi la asbestos;
§  Vumbi la fiberglass;
§  Moshi wa tumbaku;
§  Acryl-amides ambazo ni kemikali zinazopatikana kwenye vyakula vya wanga vilivyopikwa katika joto la juu sana kama chips za viazi, mikate na maandazi;
§  Heterocyclic amines ambazo ni kemikali zinazojiunda pale vyakula vya protini kama nyama vinapoungulia na kutengeneza hali ya kuwa kama mkaa;
§  Vinyl Chloride ambayo hutumika katika uzalishaji wa PVC;
§  Formaldehyde ambayo hutumiwa katika kutunzia maiti;
§  Benzene ambayo ni moja ya malighafi kubwa zinazotumiwa viwandani kwa ajili ya uzalishaji wa kemikali zinazohitajika kwa matumizi mengine mbalimbali;
§  Madini kama zebaki (mercury) na nickel; na
§  Kemikali za aina ya dioxins ambazo ni zao la ziada aghalabu pale uchomaji wa taka za majumbani na viwandani unapokuwa haukukamilika. Kemikali hizi pia huzalishwa kwa kiwango kidogo katika mchakato wa utengenezaji wa karatasi (kuzifanya ziwe nyeupe) na katika uzalishaji wa aina fulani ya kemikali zenye kiambata cha kiasili cha chlorine kama vile Polychlorinated Biphenyls (PCBs), chlorinated phenols, chlorinated benzene na baadhi ya madawa ya kuulia wadudu na wanyama waharibifu. Aidha, moshi unaotoka kwenye vipumulio vya vyombo vya usafiri (exhaust pipes), misitu inayoungua, na kuni pia huziachia kwenda hewani.
Kwa upande wa vimelea, mifano iliyozoeleka ni kama vile:
§  Aflatoxin B1, ambayo ni zao la fangasi inayoitwa Aspergillus flavus inayoota katika nafaka zilizohifadhiwa, njugu na siagi ya karanga (peanut butter);
§  Baadhi ya virusi, kama vile hepatitis B na hepatitis C vinavyohusishwa na saratani ya ini; human papilloma virus (HPV) kinachohusishwa na saratani ya shingo ya kizazi; herpesvirus 8 kinachohushwa na saratani ya ngozi; na Epstein-Barr virus kinachohusishwa na saratani aina ya lymphoma ambayo huikumba sehemu ya mfumo wa kinga za mwili inayoitwa mfumo wa lymph. 
§  Baadhi ya bakteria kama vile Helicobacter pylori ambayo inahusishwa na saratani ya tumbo pamoja na vidonda vya tumbo.
Hata hivyo ni vizuri ikaeleweka kuwa carcinogens siyo lazima zikaleta madhara kwenye seli hapohapo zinapoingia mwilini. Kuna wakati baadhi ya carcinogens hupitia njia za mzunguko kupitia mchakato au michakato kadhaa kabla ya kufanya uharibifu unaozungumziwa.

Ziko carcinogens kadhaa zinazoweza kuitwa kuwa ni za kiasili. Miongoni mwa hizi ni Aflatoxin B1, kirusi cha hepatitis B, na HPV. 

Sukari! Tafiti zimeibaini kuwa ni kianzishaji na kiendelezaji kikubwa cha saratani.

Katika utafiti uliopewa jina Increased sugar uptake promotes oncogenesis via EPAC/RAP1 and O-GlcNAc pathways na kuchapishwa tarehe 09/12/2013 katika jarida la kitaaluma la Journal of Clinical Investigation, watafiti wameonyesha kuwa sukari siyo tu kwamba ni kichocheo kikubwa cha kuongezeka na kukua kwa seli za saratani mwilini, lakini pia ni kianzilishi cha saratani katika seli ambazo hapo awali zilikuwa na siha njema.
Ni vizuri hapa ikaeleweka kuwa inapozungumzwa sukari, kinachozungumziwa ni chakula chochote ambacho kikiliwa na kuchakatwa ndani ya mwili, kina uwezo wa kusababisha ongezeko la sukari kwenye damu na hivyo kuchochea ongezeko la hormoni ya insulin ndani ya damu. Hii ina maana kuwa vyakula husika ni sukari yenyewe ya mezani na vyakula vingine vyenye uwezo huo, hususan vile ambavyo vina kiasi kikubwa cha wanga.

Tuesday, June 14, 2016

UNAPOKUWA NA UGONJWA WA KISUKARI UNAKABILIWA NA HATARI MARA 3 ZAIDI YA KUKUMBWA NA SARATANI KULIKO MTU AMBAYE HANA KISUKARI: CHUKUA HATUA!


UGONIWA WA KISUKARI NA SARATANI


Tafiti zinaonyesha kwamba kuna wakati saratani ni matokeo ya mchakato wa ukarabati wa seli zilizoharibika ndani ya mwili. Tafiti hizi zinaonyesha kwamba mimba inapotungwa seli katika mimba hiyo changa hugawanyika haraka sana na kutengeneza makundi mawili ya seli zenye maumbile na kazi tofauti. Kundi la kwanza la seli hizo (Kiini tete, au embryo kwa lugha ya kitaalamu) huendelea kugawanyika na  kubadilika likiwa safari kutengeneza kiumbe ambacho hatimaye kitazaliwa kama mtoto. Hali kadhalika kundi la pili nalo hundelea kugawanyika na kubadilika na hatimaye kutengeneza kondo la uzazi (placenta) ambalo kazi yake ni kulizingira lile kundi la kwanza.  

Kila moja ya seli katika kundi hili la seli ambalo sasa limetengeneza kondo la uzazi ina gamba ambalo limebeba umeme hasi. Seli hizi kitaalamu huitwa Trophoblasts.  Kazi ya hizi Trophoblasts ni kutoa ulinzi kwa kiini tete kisiweze kushambuliwa na mfumo wa kinga za mwili za mama! Bila seli hizi chembechembe nyeupe za damu katika mwili wa mama ambazo huunda sehemu kubwa ya jeshi la kinga katika mwili wa mwanadamu zingeshambulia kiini tete hicho na kukiharibu kwa dhana kwamba ni adui ailiyeingia mwilini! Kinachotokea ni kwamba kwa kuwa chembechembe hizi nyeupe za damu nazo zimebeba umeme hasi kama zilivyo Trophoblasts, zinapokaribia eneo kiliko kiini tete umeme hasi wa Trophoblasts na ule wa chembechembe cheupe husukumana (repels each other) na hivyo kusababisha chembechembe hizo nyeupe kusogezwa mbali na kiini tete. Tafiti zinaonyesha kuwa ulinzi huu wa Trophoblasts hukoma ghafla katika juma la nane la ujauzito. 

Tafiti zinaonyesha kuwa sababu ya hatua hii ni kwamba katika kipindi hiki kiumbe kinachoendelea kukua na kubadilika tayari kina ngongosho linalofanya kazi na kongosho hili huzalisha kiasi kikubwa cha vimeng’anyo (pancreatic enzymes) ambavyo haviruhusu trphoblasts au chembechembe nyeupe za damu kutoka kwa mama kusogea katika eneo hilo. Vimeng’enya hivi vina uwezo wa kuchakatua na kuyeyusha protini (digest) hivyo basi chembechembe yoyote nyeupe katika eneo hilo, au seli ya trophoblast itaharibiwa kwa protini yake kuchakatuliwa na kuyeyushwa na vimeng’enya hivyo.

Tafiti zinaonyesha kuwa mwili unapositisha uzalishaji wa trophoblasts, chache ya hizi seli hubakia zikiogelea kwenye damu katika kipindi chote cha maisha ya kiumbe. Kazi ya hizi trphoblasts ni kusaidia katika ukarabati wa seli za mwili zinazoharibika kwa sababu mbalimbali. Katika eneo ambalo seli zimeharibika na zinahitaji kukarabatiwa seli chache za trophoblasts huenda katika eneo hilo na kuanza kugawanyika kwa kasi inayozifanya kuongezeka kwa wingi ndani ya muda mfupi, huku zikifanya kazi ya kusadia ukarabati. Tatizo linakuja pale ambapo uharibifu wa seli husika ni kitendo endelevu na pengine cha kudumu. Kwa mfano, kwa wavutaji wa sigara wa muda mrefu ambapo uharibifu wa seli za mapafu yao ni endelevu. Hii ina maana kwamba katika eneo husika trophoblasts zitakuwa zinajigawanya kwa kasi na zitaongezeka kupindukia mipaka (out of control growth). 

Uchunguzi wa kimaabara unaonyesha kuwa seli za trophoblasts zinazojikuta katika mazingira ya aina hii hufanana kwa kila hali na seli za saratani! Hii imepelekea baadhi ya wanasayansi kuamini kuwa saratani chanzo chake ni nia nzuri na jitihada ya mwili kutaka kurekebisho kasoro zinazojitokeza katika seli za mwili. Jitihada zinapokwenda mrama kutokana na uharibifu katika seli husika kuwa endelevu basi saratani hujitokeza. Imethibitika kuwa vimeng’enyo vinavyozalishwa na kongosho (pancreatic enzymes) ni msaada mkubwa wa kuzuia trophoblasts kutengeneza saratani mwilini. 

Ugunduzi huu ulifuatia jitihada kubwa za Dr. William D. Kelly wa kule nchini Marekani ambaye aliamini kuwa saratani ni zao la mwili kushindwa kuchakatua vizuri vyakula vya jamii ya protini kutokana na upungufu wa vimeng’enya vinavyozalishwa na kongosho, hususan vile ambavyo kazi yake ni kuchakatua na kuyeyusha protini (proteolitic enzymes).

Ili kuusadia mwili kufanya kazi hiyo kwa ufanisi Dr. Kelly alipendekeza mfumo wa tiba kwa wagonjwa wake ambao ulijumuisha marekebisho katika lishe, matumizi ya tiba-lishe (nutritional suppliments), na uondoshaji wa sumu mwilini. Dr. Kelly ambaye alipingwa sana na madaktari wa mfumo (conventional cancer doctors) alisafishwa na Dr. Nicholas Gonzales wa Newyork ambaye alifanya kazi kubwa ya kutafiti kesi moja moja ya wagonjwa wa Dr. Kelly kwa udhamini wa taasisi ya Memorial Sloan - Kettering Cancer Center. Ripoti ya kazi ya Dr. Gonzales, iliyokuwa na kurasa 500, ilithibitisha kuwa tiba ya Dr. Kelly ilikuwa kweli inafanya kazi katika saratani za aina nyingi mwilini. 

Utafiti wa ziada uliofanywa katika kazi ya Dr. Kelly na wengine waliomfuata umethibitisha bila shaka kuwa uchache wa vimeng’enya vya kongosho ni sababu ya msingi ya kuibuka kwa saratani mwilini; na kuwa wagonjwa wa ugonjwa wa kisukari ambao kimsingi kongosho zao zinazalisha kiwango kidogo cha hivi vimeng’enya, wako katika hatari mara tatu zaidi ya kupata ugonjwa wa saratani.

Hii ina maana kuwa mgonjwa wa kisukari anatakiwa achukue tahadhari mara tatu zaidi kuliko mtu wa kawaida katika kulinda seli zake za mwili zisiharibike na kujenga mazingira ya trophoblasts kuzaliana kwa wingi. Uharibifu huu ni ule unaoweza kufanywa na uvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula vilivyotunzwa kwa kemikali, matumizi ya vipodozi bandia (synthetic cosmetics), matumizi ya nyama zilizochakatuliwa na kuhifadhiwa kwa kemikali, matumizi ya nyama za kuchoma zilizoungulia na kufanya mkaa, nakadhalika. Aidha mgonjwa wa sukari anahitaji kutumia nyongeza/tiba- lishe (nutritional supplements) za vimeng’enya, hususan vile ambavyo kazi yake kubwa ni kuchakatua na kuyeyusha protini. 


KISUKARI CHA UKUBWANI NI RAHISI KUTIBIKA – ELEKEZA JITIHADA KATIKA KUDHIBITI MFURO (INFLAMMATION)




Mfuro ni kitu gani?

Umeshawahi kujikwaa ukiwa hukuvaa viatu? Au umeshawahi kujigonga/kugongwa kwa nguvu kidogo, hasa kichwani au kwenywe paji la uso? Inawezekana baada ya matukio haya ulishuhudia uvimbe katika vidole vya mguu, au nundu katika kichwa au paji lako la uso. Basi huo ni mfuro.

Ukiachilia mbali mifuro inayosababishwa na kujiumiza kimwili moja kwa moja kama tulivyoeleza katika hiyo mifano hapo juu, seli zetu za mwili kuanzia za ndani hadi zile za nje huweza kupatwa na mfuro kwa sababu nyingine mbalimbali.

Kwa kawaida kinga za mwili zinapoingia kupambana na kitu chochote kile zinachikidhania ni hatari kwa mwili, moja ya matokeo katika eneo la mapambano ni mfuro. Hii ina maana kwamba kila unapopata maambukizi yoyote yale, pamoja na ugonjwa wenyewe unaosababishwa na hayo maambukizi, sehemu ya maamivu unayokabiliana nayo hutokana na kuenea kwa mfuro mwilini. 

Kwa bahati mbaya sana maisha ya kisasa yametawaliwa na vitu vingi sana vinavyosababisha kinga za mwili ziwe katika mkao wa vita muda wote.  Vitu hivi ni pamoja na baadhi ya vyakula; vinywaji ; dawa (hususan zile za kifamasia); na vipodozi. Baadhi ya vitu hivi vinapoingia ndani ya mwili huchochea kinga za mwili kudhani kuwa adui kaingia; na kwa hivyo moja kwa moja huingia katika mapambano. Kwa kuwa vitu hivi tunakutana navyo kila siku na kila mara, hii ina maana kuwa miili yetu inakabiliwa na mfuro karibu muda wote. Inaaminika kuwa miongoni mwa vyakula vinavyochochea mfuro kwa kiwango cha juu sana ni nafaka zote zilizochakatwa (kuondoa ganda la juu); sukari; na mafuta yanayotokana na mbegu pale yanapotumiwa kwa matumizi ya kupikia.  Mafuta ya mbegu ni pamoja na yale ya alizeti, ufuta, mawese, karanga, pamba, nakadhalika.

Kitu kingine kinachosababisha mfuro endelevu ni mtindo wa maisha wa kubweteka. Kiasili hatukuumbwa tuwe ni watu wa kutulia eneo moja kwa muda mrefu.  Maumbile yetu yanahitaji viungo vyetu viwe vinajongea muda mwingi pale tunapokuwa tuko macho. Tafiti zimebainisha kuwa kuketi au kujilaza sehemu moja muda mrefu (nusu saa au zaidi) kunauingiza mwili uwe katika hali ambayo inasababisha mfuro katika seli. Moja ya namna za kutambua kiwango cha mfuro mwilini ni kupima kiwango cha chembechembe zinazoitwa C- Reactive Protine (CRP). Tafiti zinaonyesha kuwa CRP inaongezeka katika mzunguko wa damu kwa kitendo cha kuketi tu sehemu moja kwa muda mrefu.

Madhara ya Mfuro.

Umeshawahi kukutana na tukio la kusumbuliwa na mlango wa mbao wakati wa kuufunga au kuufungua, hususan wakati wa msimu wa mvua? Kuna baadhi ya mbao zina tabia ya kunyonya unyevu unyevu na kufura. Milango au madirisha yanayotengenezwa na aina hii ya mbao mara nyingi inaweza ikasumbua wakati wa  kufunga au kufungua wakati wa vipindi vya mvua endelevu.  Mfano huu ni sawa na kinachotokea kwenye seli inayokabiliwa na mfuro.

Kila seli ina vitu vinavyoitwa ‘vipokezi’ au kwa kitaalamu cell receiptors. Vipokezi hivi ni sawa na milango na madirisha. Moja ya kazi ya vipokezi hivi ni kupokea viini-lishe, maji na gesi ya oxygen kutoka nje ya seli na kuviingiza ndani ya seli kwa ajili ya majukumu mbalimbali.  Kazi nyingine ni kutoa nje ya seli uchafu wa mabaki ya viini-lishe, maji yaliyotumika na hewa chafu kwa ajili ya kuondolewa mwilini. 

Vipokezi kwenye seli yenye mfuro ni sawa na mbao ya dirisha au mlango inayonyonya unyevu nyevu.  Mfuro hupelekea vipokezi hivi visifanye kazi kwa ufanisi. Wataalamu wengi wanaamini kuwa kutokana na hali ya miili yetu kukabiliwa na mfuro ambao ni endelevu, ufanisi wa vipokezi katika seli zetu uko chini sana na hali hii ndiyo chimbuko kubwa la maradhi mengi ya kimfumo, ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa kisukari.

Chukua Hatua Kukabiliana na Mfuro

Hatua muhimu katika kukabiliana na mfuro ni pamoja na:
  1. Kuacha kula vyakula vinavyochochea mfuro. Kama ambavyo tumekwishaona, vyakula hivi ni vile  vyote vinavyotokana na nafaka zilizochakatwa. Vingine ni SUKARI na vile vilivyopikwa kwa mafuta ya mbegu, yaani vegetable oils;
  2. Kuvifanya viungo vyote vya mwili viwe katika hali ya kujongea (move) kila mara. Ni vema kutoruhusu kuketi sehemu moja kwa muda unaozidi nusu saa. Nyanyuka, jinyooshe, tembea hatua mbili tatu, kisha rejea kwenye kiti chako kila baada ya muda fulani. Mazoezi ya viungo ya walau siku nne kwa wiki ni msaada mkubwa. Hata hivyo pale ambapo fursa ya kufanya mazoezi ni finyu, ni muhimu kutenga muda kila siku na kutembea kwa mguu kiasi cha kiliometa tatu au nne;
  3. Hakikisha unajitibu magonjwa yote ya maambukizi yaliyoko mwilini mwako; na
  4. Jenga tabia ya kula au kunywa vitu vyenye sifa ya kukabiliana na mfuro. Baadhi ya vitu hivi ni pamoja na:
    1. Viungo kama manjano; tangawizi; karafuu; jira (binzari nyembamba); na habat Sauda (black seed);
    2. Chai ya kijani (green tea); na
    3. Matunda kama zabibu, zambarau